
Mwanamuziki maarufu duniani Madonna amewaacha mashabiki wengi wakiwa na hofu kubwa baada ya kning’inia kwenye kingo za jukwaa akiwa kwenye tamasha la kushtukiza la Pride lililofanyika katika Times Square nchini Marekani.
Madonna mwenye umri wa miaka 67 alikuwa akitumbuiza katika tamasha lililoandaliwa na Grindr, ambapo jukwaa lake lilikuwa limejengwa juu sana kutoka usawa wa ardhi huku maelfu ya mashabiki wakishuhudia tukio hilo moja kwa moja.
Katika moja ya matukio yaliyowashtua wengi, Madonna alionekana akivuka sehemu ya kinga ya kioo iliyowekwa pembeni mwa jukwaa na kutundika mguu mmoja nje ya ukingo huo, hali iliyowafanya mashabiki wengi kuhofia usalama wake.

Video zilimuonesha mwanamuziki huyo akiwa karibu kuning’inia juu ya umati mkubwa wa watu waliokuwa chini ya jukwaa, jambo lililosababisha mashabiki wengi kuelezea hofu yao kupitia mtandao wa X.
Baadhi yao waliandika:
“Madonna usifanye hivyo!”
wakati wengine wakisema:
“Nilihofia sana,”
“Karibu nipate presha kwa tukio lile.”
Akiwa amevaa mavazi ya corset yenye rangi ya pinki na bluu pamoja na buti ndefu, Madonna aliimba nyimbo kadhaa kutoka albamu yake mpya Confessions II inayotarajiwa kutoka Julai 3 mwaka huu.

Katika tamasha hilo pia aliambatana na DJ na mtayarishaji wa muziki kutoka Uingereza Stuart Price ambaye amefanya kazi naye kwa muda mrefu tangu albamu yake ya Confessions on a Dance Floor ya mwaka 2005.
Mbali na burudani, tamasha hilo lilikuwa na sehemu maalum ya kuenzi historia ya harakati za haki za mashoga kupitia picha mbalimbali zilizooneshwa jukwaani huku Madonna akiwa pamoja na wachezaji wake wa nyuma.