
Siku chache zilizopita, video ilianza kusambaa mitandaoni ikimuonesha mama lishe mmoja akihudumia wateja wengi waliomzunguka katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam. Video hiyo ilizua gumzo kubwa na kuvuta hisia za watu wengi kwenye mitandao ya kijamii.
Kutokana na video hiyo kusambaa kwa kasi, Global TV ilifanikiwa kumtafuta na kumfikia mama huyo nyumbani kwake, eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam, ili kujua zaidi kuhusu maisha yake na shughuli zake za biashara.

Mama huyo anajulikana kwa jina la Afua Juma, ingawa wateja wake wengi wanamfahamu zaidi kwa jina la “Mama Manyema.” Amejijengea umaarufu mkubwa kutokana na huduma zake za chakula anazotoa katika Mtaa wa Manyema, Kariakoo, ambapo hupata wateja wengi kila siku.
Biashara yake imeendelea kukua kutokana na uaminifu na huduma nzuri kwa wateja wake, jambo ambalo limechangia pia jina lake kusambaa zaidi mitandaoni baada ya video hiyo ya hivi karibuni.
Afua Juma amesema anaendelea kujituma katika biashara yake ya mama lishe huku akishukuru wateja wake kwa sapoti kubwa wanayompa kila siku katika shughuli zake za kujipatia kipato.