×

Mabadiliko ya Tabianchi Yaendelea Kutishia Uchumi wa Tanzania

Kadri changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinavyoendelea kuongezeka duniani ndivyo amabvyo kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) inaendelea kuonesha jinsi sekta binafsi inaweza kuwa sehemu ya suluhisho.

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani 2026 chini ya kaulimbiu ya “Inspired by Nature. For Climate. For Our Future” (Tukihamasishwa na Asili kwa Ajili ya Tabianchi na Mustakabali Wetu),  na kwa Tanzania kauli mbiu ikiwa ni ‘Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania’, mjadala kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaendelea kuhama kutoka kwenye kuongeza uelewa kuelekea kuchukua hatua za vitendo.

Kwa nchi kama Tanzania, umuhimu wa hatua hizo hauwezi tena kupuuzwa.

Ingawa Tanzania inachangia takribani asilimia 0.31 pekee ya uzalishaji wa gesi joto duniani, bado ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kupunguza ukuaji wa uchumi kwa hadi asilimia 4 ifikapo mwaka 2050, kusababisha watu milioni 2.6 kuingia kwenye umaskini na kuwafanya mamilioni kuhama makazi yao iwapo hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hizo hazitachukuliwa.

Katika bara la Afrika, hali nayo inatia wasiwasi. Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) linakadiria kuwa matukio yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi tayari yanagharimu uchumi wa nchi za Afrika kati ya asilimia 2 hadi 5 ya Pato la Taifa (GDP) kila mwaka, jambo linaloongeza shinikizo kwa serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.

Changamoto hii ni kubwa zaidi kwa Tanzania ambapo sekta ya kilimo inachangia takribani asilimia 26 ya Pato la Taifa na kutoa ajira kwa karibu asilimia 65 ya nguvu kazi ya nchi. Kadri mifumo ya mvua inavyoendelea kubadilika na rasilimali za maji kuwa na uhaba, athari zake zinaendelea kujitokeza katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo.

Kutokana na hali hiyo, wataalamu wengi wanaamini kuwa juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi haziwezi kuachiwa serikali pekee. Sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuendeleza uhifadhi wa mazingira sambamba na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi.

Miongoni mwa kampuni zilizoweka mkazo katika ajenda hiyo ni Serengeti Breweries Limited (SBL).

Baada ya kujiunga na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Uwajibikaji wa Kampuni Duniani (United Nations Global Compact), SBL imeendelea kujumuisha masuala ya uendelevu katika mkakati wake wa biashara, hususan katika maeneo ya uhifadhi wa rasilimali za maji na kilimo endelevu.

Uwekezaji Katika Usalama wa Maji

Maji ni mojawapo ya rasilimali muhimu zaidi kwa maisha ya jamii na maendeleo ya viwanda. Kwa kutambua umuhimu huo, SBL imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 2.5 katika miradi ya maji kwa jamii kupitia programu yake ya Water for Life.

Kupitia programu hiyo, zaidi ya Watanzania milioni 2.3 wamepata huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini. Mbali na kuboresha afya za wananchi, miradi hiyo imechangia kupunguza mzigo kwa wanawake na watoto ambao mara nyingi hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, huku ikiongeza uwezo wa jamii kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji.

Sambamba na uwekezaji huo kwa jamii, kampuni imeendelea kuboresha matumizi bora ya maji na nishati katika shughuli zake za uzalishaji, ikionesha kuwa uhifadhi wa mazingira unaweza kwenda sambamba na mafanikio ya biashara.

Kujenga Kilimo Chenye Ustahimilivu Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi

Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, lakini pia ni miongoni mwa sekta zilizoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Kama mnunuzi mkubwa wa mazao yanayozalishwa nchini, SBL inashirikiana na wakulima katika mikoa mbalimbali na kuendelea kuwekeza katika programu zinazohamasisha kilimo endelevu.

Kupitia mpango wa Shamba ni Mali, wakulima hupatiwa mafunzo na usaidizi unaolenga kuongeza tija huku wakihamasishwa kutumia mbinu za kilimo himilivu zinazowasaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Aidha, kampuni imewekeza katika kuandaa kizazi kijacho cha wataalamu wa kilimo kupitia programu ya Kilimo Viwanda, ambayo imekuwa ikiwasaidia vijana wa Kitanzania wanaosomea na kujikita katika sekta ya kilimo.

Kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, vijana 300 wamepatiwa mafunzo kuhusu mbinu za kisasa na himilivu za kilimo. Vijana hao, waliotoka katika maeneo mbalimbali nchini, wanaendelea kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwafikia na kuwasaidia wakulima wengine katika maeneo yao.

Mipango hii inatambua kuwa mafanikio ya muda mrefu ya biashara yanategemea ustawi wa wakulima, jamii na mifumo ya ikolojia inayozalisha malighafi muhimu kwa kampuni.

Wajibu wa Pamoja

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu yanatoa wito kwa serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kuondoka kwenye hatua ya kutambua changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuanza kuchukua hatua madhubuti za kulinda mazingira chini ya kaulimbiu ya “Inspired by Nature. For Climate. For Our Future.”

Ni wazi kuwa sekta binafsi pekee haiwezi kutatua changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Ingawa ina rasilimali na uwezo wa kuchochea suluhisho kwa kasi zaidi, kukabiliana na changamoto hii kunahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Kadri Siku ya Mazingira Duniani 2026 inavyoangazia umuhimu wa suluhisho zinazotokana na asili, uzoefu wa SBL unaonesha jinsi uwekezaji wa sekta binafsi unavyoweza kuchangia uhifadhi wa mazingira huku ukiendelea kuleta manufaa ya kijamii na kiuchumi.

Safari ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi bado ni ndefu. Hata hivyo, kadri changamoto hizi zinavyoendelea kuongezeka, ushirikiano kati ya serikali, jamii, mashirika ya maendeleo na sekta binafsi utakuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Kwa Tanzania, kujenga mustakabali wenye ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kunahitaji mchango wa kila sekta. Kwa sasa, sekta binafsi inaendelea kuonesha kuwa inaweza kuwa sehemu muhimu ya suluhisho hilo.

Leave a Comment