
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Marekani itaishambulia Iran kwa nguvu kubwa usiku wa leo, huku pia akiahidi kuchukua udhibiti wa Kisiwa cha Kharg na miundombinu mingine muhimu ya mafuta na gesi ya nchi hiyo.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alidai kuwa uwezo mkubwa wa kijeshi wa Iran, ikiwemo jeshi la wanamaji, jeshi la anga na mifumo ya ulinzi wa anga, tayari umedhoofishwa na mashambulizi yaliyopita. Pia alisisitiza kuwa Marekani itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya iran.

Trump aliongeza kuwa katika siku zijazo Marekani itachukua udhibiti wa Kisiwa cha Kharg, ambacho ni kitovu muhimu cha usafirishaji wa mafuta ya Iran, pamoja na maeneo mengine ya miundombinu ya nishati.
Kauli hiyo imeongeza hofu ya kuongezeka kwa mvutano katika Mashariki ya Kati, wakati Marekani na Iran zikiendelea kubadilishana mashambulizi licha ya juhudi za kidiplomasia za kufikia makubaliano ya amani na masuala ya nyuklia.
Kisiwa cha Kharg kinatajwa kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi kwa uchumi wa Iran kwani hupitisha sehemu kubwa ya mauzo ya mafuta ghafi ya nchi hiyo kwenda soko la kimataifa.
Kauli za Trump zimekuja wakati dunia ikiendelea kufuatilia kwa karibu mwelekeo wa mgogoro huo, ambao unaweza kuwa na athari kubwa kwa usalama wa kikanda na soko la mafuta duniani.
