
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kumpata mtoto Razaki Damas Mwakatundu (5), mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya Mwakikome iliyopo Wilaya ya Kyela, ambaye alikuwa ametekwa kwa takribani siku 13 na mtu anayetajwa kuwa baba yake mlezi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo lilitokea Juni 1, 2026 katika Kata ya Katumbasongwe, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, ambapo mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake nyumbani kwao kabla ya baba yake mlezi kufika na kumchukua kisha kutoweka naye kwenda kusikojulikana.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alikuwa akishinikiza kurejeshewa kiasi cha shilingi 550,000 alichodai kuwa alitoa kama mahari kwa mama wa mtoto huyo. Inadaiwa mama huyo alikataa kuolewa naye licha ya kupokea fedha hizo.
Baada ya taarifa kutolewa Polisi na kufunguliwa kwa kesi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Kikosi Maalum cha Kuzuia na Kupambana na Uhalifu lilianzisha msako mkali wa kumtafuta mtoto huyo pamoja na mtuhumiwa.
Juni 14, 2026, juhudi hizo zilizaa matunda baada ya mtoto huyo kupatikana akiwa hai katikati ya msitu wa Hifadhi ya Kitulo uliopo mpakani mwa mikoa ya Mbeya na Njombe, ambako alidaiwa kutelekezwa.
Polisi wamesema msako mkali bado unaendelea ili kumkamata mtuhumiwa huyo anayeshukiwa kumteka na baadaye kumtelekeza mtoto huyo baada ya kubaini kuwa alikuwa akifuatiliwa na vyombo vya usalama.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na wahalifu wengine wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika jamii.