×

Diddy Apunguziwa Muda wa Kifungo kwa Mara Nyingine Marekani

Msanii na mfanyabiashara maarufu wa muziki Sean Combs.

Msanii na mfanyabiashara maarufu wa muziki Sean Combs, anayejulikana pia kama Diddy, ameongezewa tena punguzo la muda wake wa kifungo huku tarehe yake ya kuachiliwa gerezani ikisogezwa mbele hadi Februari 23, 2028.

Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Magereza ya Marekani (Federal Bureau of Prisons), hii ni mara nyingine tena tarehe yake ya kuachiliwa kubadilishwa. Hapo awali alikuwa anatarajiwa kutoka Aprili 15, 2028, kabla ya tarehe hiyo kusogezwa kutoka Aprili 25 na baadaye Juni 4, 2028.

Diddy, mwenye umri wa miaka 56, anahudumia kifungo cha miezi 50 katika gereza la FCI Fort Dix baada ya kupatikana na hatia mwaka jana kwa makosa mawili ya kusafirisha watu kwa ajili ya kujihusisha na ukahaba. Hata hivyo, aliachiliwa huru katika mashtaka mazito zaidi yaliyokuwa yakimhusisha na biashara ya ngono na njama za uhalifu wa kupangwa.

Ripoti zinaeleza kuwa Diddy amekuwa akishiriki katika programu ya tiba na urekebishaji wa matumizi ya dawa za kulevya akiwa gerezani. Wanasheria wake waliomba apelekwe katika gereza hilo kutokana na uwepo wa programu hizo pamoja na ukaribu wake na familia.

Pamoja na kupunguziwa muda wa kifungo, vita yake ya kisheria bado haijaisha. Timu yake ya mawakili imekata rufaa kupinga hukumu na adhabu aliyopewa, ikidai kuwa mahusiano yaliyokuwa msingi wa kesi hiyo yalikuwa ya hiari na kwamba kifungo alichopewa ni kikubwa kupita kiasi.

Katika nyaraka za rufaa zilizowasilishwa mwezi Machi, mawakili wa Diddy walieleza hukumu hiyo kuwa ni upotoshaji wa haki na kuomba aachiliwe huru mara moja au apewe hukumu mpya.

Kwa upande mwingine, waendesha mashtaka wa serikali ya Marekani wameiomba mahakama ya rufaa kutupilia mbali madai hayo, wakisisitiza kuwa jaji aliyetoa hukumu alizingatia ushahidi wote uliowasilishwa wakati wa kesi.

Kwa sasa, rufaa hiyo bado inasikilizwa katika mahakama ya rufaa ya shirikisho nchini Marekani jambo linalomaanisha kuwa hatima ya mwisho ya Diddy bado haijajulikana licha ya tarehe yake ya kuachiliwa kuendelea kusogezwa mbele.

Leave a Comment