×

Video: Wachina Wanaodaiwa Kumteka Mwenzao Wafikishwa Mahakamani

Wafanyabiashara Raia wanne wa China, Deng Anqing, Fan Zhong Hua, Zhang Jianjun na Deng Qiang, wamekosa kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Kinyerezi jijini Dar es Salaam baada ya kukosekana kwa mkalimani wa mahakama.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Herieth Mwailolo kwa ajili ya kusomewa mashitaka ya uhujumu uchumi, lakini zoezi hilo lilishindikana kwa sababu wote hawajui Kiswahili wala Kiingereza, hivyo mahakama ikashindwa kuendelea na shauri hilo.

Hakimu Mwailolo ameahirisha kesi hiyo namba 13626/2026 hadi kesho, akielekeza Mahakama kuhakikisha inampata mkalimani ili washtakiwa hao waweze kusomewa mashtaka yao na kuelewa kinachoendelea.

Ikumbukwe kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam lilitangaza kuwakamata Watu wanne raia wa China kwa tuhuma za utekaji wa Wafanyabiashara wawili ambao ni Wachina wenzao.

Wafanyabiashara hao wanadaiwa walitekwa katika majengo pacha ya PSSSF jijini Dar es salaam na waliokolewa na Jeshi la Polisi baada ya operesheni maalumu iliyofanyika Mei 16, 2026.

Kamanda Muliro alisema Mei 14, 2026 saa 7:30 usiku polisi walipokea taarifa za kutekwa kwa Weiyi Chen (64) na Liang Xiolo (44), ambao ni wafanyabiashara na raia wa China.

Leave a Comment