×

Polisi Adaiwa Kumuua Aliyekataa Kumpa Rushwa

OFISA mmoja wa polisi amekamatwa akituhumiwa kumuua kwa kumpiga risasi dereva wa gari aina ya Probox baada ya dereva huyo kukataa kumpa rushwa katika tukio lililotokea kwenye barabara ya Pusangi-Esoit katika Kaunti ya Narok , nchini Kenya, jana.

 

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Transmara-Magharibi, Dahir Abdulahi,  amesema aliyeuawa alikuwa na miaka 21 na kuongeza kuwa mshtakiwa alijisalimisha katika kituo cha Esoit na baadaye kuhamishiwa Kituo cha Polisi Kilgoris.

 

Inadaiwa dereva na bosi wake wakiwa ndani ya Probox walikuta mawe yamepangwa barabarani. APC Wilson Kortom aliwasimamisha na kisha inadaiwa aliwaomba rushwa kutokana na mkaa waliokuwa wakiusafirisha ndani ya gari.

 

Inadaiwa kulitokea kutoelewana na dereva alishuka kwenye gari na kwenda kutaka kutoa mawe barabarani na ndipo polisi alipotoa bastola na kumpiga dereva kifuani kisha kuondoka na pikipiki yake.

 

Polisi imesema imeanza uchunguzi wa tukio hilo huku ikikanusha kuwa hakukuwa na mkaa kwenye gari hilo kwani matokeo ya awali ya uchunguzi yanaonyesha gari hilo halikubeba kitu.

Leave a Comment