×

Waziri Mkuu wa Italia Akataa Madai ya Trump, Asema Ni Uongo wa Kutungwa

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni akiongea jambo na Rais wa Marekani, Donald Trump wakati wa mkutano wa viongozi wa nchi tajiri duniani wa G7.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, amemjibu kwa ukali Rais wa Marekani, Donald Trump, baada ya kudai kuwa aliomba kupigwa picha naye wakati wa mkutano wa viongozi wa nchi tajiri duniani wa G7.

Meloni amekanusha madai hayo akiyataja kuwa ya kubuniwa kabisa, huku akisema ameshangazwa na kauli za Trump dhidi ya mshirika wa karibu wa Marekani.

“Nimeshtushwa kwa kweli. Sijui kwa nini Rais wa Marekani anawatendea washirika wake kwa namna hii. Hii si mara ya kwanza kutokea,” alisema Meloni katika video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Kiongozi huyo wa Italia alisisitiza kuwa yeye binafsi na taifa la Italia hawajawahi kuomba upendeleo wa aina hiyo.

“Kuna jambo moja anapaswa kukumbuka. Wala mimi wala Italia hatuombi,” alisema.

Mzozo huo ulianza baada ya Trump kudai katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Italia kuwa Meloni alimwomba wapige picha pamoja wakati wa mkutano wa G7.

Kwa mujibu wa Trump, angeweza kukataa ombi hilo lakini alikubali kwa sababu alimhurumia Waziri Mkuu huyo wa Italia. Kauli hizo zimezua mjadala mkubwa nchini Italia na katika medani za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani, naye ameonyesha kutoridhishwa na kauli za Trump, akitangaza kufuta safari yake iliyokuwa imepangwa kuelekea Marekani.

Tajani alisema matamshi ya Trump dhidi ya Meloni ni ya kuudhi na hayamlengi Waziri Mkuu pekee bali taifa lote la Italia.

“Kauli za Rais Trump dhidi ya Giorgia Meloni zinawakera Waitalia wote,” alisema Tajani.

Mahusiano kati ya Trump na Meloni yamekuwa yakikumbwa na misuguano mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, licha ya viongozi hao wawili kuonekana mara kadhaa wakishirikiana katika mikutano ya kimataifa.

Tukio hilo limeongeza mvutano mpya kati ya Washington na Roma, huku wachambuzi wakifuatilia kwa karibu athari zake katika uhusiano wa kisiasa kati ya Marekani na Italia.

Leave a Comment