
Timu ya Taifa ya Ujerumani usiku wa kuamkia leo Juni 21, 2026 imefuzu hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 2014 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ivory Coast katika mchezo mkali wa Kundi E uliochezwa jijini Toronto.
Shujaa wa Ujerumani alikuwa mshambuliaji Deniz Undav aliyefunga mabao yote mawili baada ya kuingia akitokea benchi, na kuipa timu yake ushindi muhimu uliowapeleka moja kwa moja hatua ya 32 bora.
Ivory Coast walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Franck Kessié katika kipindi cha kwanza baada ya kumalizia mpira uliotokana na shambulizi lililoanzishwa na Amad Diallo.
Licha ya Ujerumani kutawala sehemu kubwa ya mchezo na kufunga mabao mawili yaliyokataliwa na mwamuzi katika kipindi cha kwanza, waliendelea kupambana hadi dakika za mwisho.
Undav alisawazisha dakika ya 68 kwa shuti kali la volley kabla ya kufunga bao la ushindi katika muda wa nyongeza, akimalizia pasi nzuri kwa ustadi mkubwa na kumuacha kipa Yahia Fofana hana la kufanya.
Kocha wa Ujerumani, Julian Nagelsmann, aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi mwisho na kuonyesha moyo wa ushindani.
Kwa ushindi huo, Ujerumani imefikisha pointi sita na kuongoza Kundi E, huku ikihakikisha nafasi ya kucheza hatua ya mtoano. Ivory Coast imebaki na pointi tatu na italazimika kupambana katika mchezo wake wa mwisho wa kundi.