
MWANAMITINDO, mjasiriamali na mshawishi wa mitandao ya kijamii, Hamisa Mobetto, ameeleza furaha yake baada ya kuibuka mshindi wa tuzo za Influencer of the Year na Fashion Icon of the Year.
Ushindi huo umepokelewa kwa pongezi nyingi kutoka kwa mashabiki wake ambao wameeleza kuwa Hamisa anastahili tuzo hizo kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya mitindo, biashara na ushawishi wa mitandao ya kijamii. Wengi wamemtaja kuwa mmoja wa watu mashuhuri wanaovutia zaidi nchini, huku akiendelea kuwa balozi wa kampuni mbalimbali na mfano wa mafanikio kwa vijana wengi.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Hamisa alisema kuwa ushawishi wa mitandao ya kijamii umeendelea kuwa nguzo muhimu katika ukuaji wa biashara na uchumi wa kidijitali.
“Katika dunia ya leo, influencer marketing siyo tena burudani pekee; imekuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa biashara, uundaji wa ajira, na uchumi wa kidijitali. Kwa miaka kadhaa nimepata nafasi ya kushirikiana na brands mbalimbali, kusaidia biashara kufikia wateja wapya, na kuonyesha kwamba ushawishi unaweza kuleta matokeo halisi kwa jamii na uchumi wetu,” alisema Hamisa.
Aidha, aliwashukuru mashabiki wake, washirika wa biashara na timu yake kwa mchango wao katika mafanikio hayo.
“Ninashukuru sana kupokea tuzo za Influencer of the Year na Fashion Icon of the Year. Heshima hii si yangu peke yangu, bali ni ya kila mtu aliyekuwa sehemu ya safari hii. Asanteni mashabiki wangu kwa upendo na sapoti yenu isiyoisha. Asanteni washirika wangu wa biashara, brands na wadau wote wanaoendelea kuniamini,” aliongeza.
Hamisa alisema tuzo hizo ni uthibitisho kwamba bidii, nidhamu na ushirikiano vinaweza kuleta mafanikio makubwa, huku akisisitiza kuwa safari yake bado inaendelea.
“Tuzo hizi ni ushahidi kwamba kazi, nidhamu na ushirikiano vinaweza kuleta matokeo makubwa. Asanteni sana. Safari inaendelea,” alisema.