
Jamii ya Ruguruni, Kata ya Kwembe wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam imekumbwa na mshtuko mkubwa baada ya kijana mwenye umri wa miaka 21 kukiri kuwaua baba yake pamoja na babu yake katika tukio linalotikisa hisia za wengi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na Global TV, siri hiyo ilianza kufichuka baada ya ndugu na majirani kugundua sehemu ya sakafu ya nyumba ikiwa imechimbwa na kufukiwa upya kwa mchanga, jambo lililozua mashaka makubwa.
Haikuchukua muda mrefu ndipo kijana huyo alipodaiwa kujitokeza akiwa ameshika chupa ya juisi aliyodai kuwa ndiyo aliyomtumia babu yake kabla ya kufariki, huku akidai kuwa ilikuwa imewekewa sumu. Kauli hiyo ilifungua ukurasa mpya wa uchunguzi na kuibua ukweli wa kutisha uliokuwa umefichwa kwa siku kadhaa.
Mashuhuda wanasema familia ilikuwa ikimtafuta baba wa kijana huyo kwa zaidi ya wiki moja bila mafanikio, huku ikishirikiana na Jeshi la Polisi na hospitali mbalimbali. Wakati jitihada hizo zikiendelea, babu wa familia alifariki dunia na kuzikwa, bila ndugu kujua kuwa nyuma ya pazia kulikuwa na siri nzito iliyokuwa ikisubiri kufichuka.
Baada ya mwanamke mmoja kugundua damu kwenye godoro pamoja na harufu isiyo ya kawaida ndani ya nyumba, mashaka yaliongezeka. Kijana huyo alidaiwa kuwazuia ndugu kuingia ndani ya nyumba, hali iliyowafanya waanze kuhisi kuna jambo kubwa lilikuwa linafichwa.
Ni nini kilimsukuma kijana huyu kufikia hatua ya kuwaua watu wake wa karibu? Uchunguzi wa polisi umebaini nini? Na majirani pamoja na ndugu wanasemaje kuhusu maisha yake kabla ya tukio hili la kutisha?
Usikose kutazama video kamili ya Global TV, ambapo Imelda Mtema anakuletea simulizi kamili, ushuhuda wa mashuhuda, maelezo ya ndugu na taarifa za uchunguzi zinazoendelea kuhusu moja ya matukio yaliyolishtua zaidi jijini Dar es Salaam.