Waziri wa Mazingira wa Sweden, Romina Pourmokhtari, amevutia hisia za wengi baada ya kuhudhuria mkutano wa Mawaziri wa Umoja wa Ulaya (EU) uliofanyika mjini Luxembourg akiwa amembeba mtoto wake wa miezi mitatu, Adam.
Kwa mujibu wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, tukio hilo linaweka rekodi mpya kwani ni mara ya kwanza mtoto mchanga kushiriki katika mkutano rasmi wa mawaziri wa umoja huo. Romina amesema hatua hiyo imelenga kuonyesha kuwa wazazi, hasa wanawake, hawapaswi kulazimika kuchagua kati ya kutimiza majukumu ya kazi na kulea familia zao.
Ameeleza kuwa mfumo wa likizo ya uzazi uliopo nchini Sweden pamoja na ushirikiano wa mume wake vimemwezesha kurejea kazini huku mtoto akiendelea kupata malezi stahiki.
Romina, mwenye umri wa miaka 30, aliingia kwenye historia ya Sweden mwaka 2022 baada ya kuwa mmoja wa mawaziri vijana zaidi kuwahi kuteuliwa serikalini. Baada ya kumaliza likizo yake ya uzazi, amerejea kazini huku mume wake akiendelea kutumia likizo ya malezi ya mtoto wao.
Hatua yake imezua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa sera zinazowajali wazazi wanaofanya kazi na kuimarisha uwiano kati ya kazi na maisha ya familia. Baadhi ya viongozi wa Ulaya wameisifu kama mfano mzuri wa kuhamasisha mazingira jumuishi yanayowawezesha wazazi kutekeleza majukumu yao ya kikazi bila kuathiri malezi ya watoto.