
Askari wa Depo ya mwaka 2015/2016, maarufu kama J.1, wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe wameadhimisha miaka 10 ya utumishi wao kwa kugusa maisha ya wazazi waliojifungua katika Hospitali ya Vwawa, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.

Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, alisema askari hao walichagua kutembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali muhimu katika maeneo matatu; kwa mtoto mwenye ulemavu, watoto waliotelekezwa pamoja na wazazi waliojifungua. Alisema hatua hiyo ni ishara ya upendo na mshikamano kwa jamii, akibainisha kuwa kuwasaidia wenye uhitaji ni sehemu ya wajibu wa Jeshi la Polisi kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya askari hao, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Neema Minja alisema maadhimisho hayo yamekuwa fursa ya kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kufikisha miaka 10 ya utumishi, huku wakiamua kusherehekea kwa kugusa maisha ya watu wenye uhitaji katika jamii.

Kwa upande wake, Katibu wa Hospitali ya Vwawa, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Liti Jomo, aliwashukuru askari hao kwa kuwakumbuka watoto hao pamoja na wazazi waliojifungua. Alisema kitendo hicho ni cha mfano na kinapaswa kuigwa na wengine. Aidha, aliwatakia askari hao kila la heri katika kuendelea na utumishi wao, akisisitiza kuwa hatua hiyo isiwe mwisho wa matendo mema, bali iwe mwanzo wa ushirikiano endelevu kati ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe na jamii katika kuwahudumia wenye mahitaji maalumu.