
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika na taasisi za umma kuweka mikakati madhubuti ya kujiendesha kwa ufanisi na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini, ili yaweze kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo, Juni 30, 2026, wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka mashirika ya umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kwa mashirika ambayo bado hayajaanza kutoa gawio kwa Serikali kujitathmini na kujifunza kutoka kwa yale yanayofanya vizuri, ili yaweze kuimarisha utendaji wake na kuchangia zaidi mapato ya Serikali.

Katika hafla hiyo, Rais Samia amepokea jumla ya shilingi trilioni 1.327 kama gawio na michango kutoka mashirika ya umma yaliyo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) pamoja na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.
Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka 2025, ambapo Serikali ilipokea shilingi trilioni 1.028.
Akitoa taarifa kuhusu makusanyo hayo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema mashirika na kampuni za kibiashara zimechangia shilingi bilioni 800, sawa na asilimia 60 ya makusanyo yote.

Aidha, amesema michango ya mapato ghafi kutoka taasisi imefikia shilingi bilioni 406, sawa na asilimia 30 ya makusanyo yote, huku mapato mengine yakichangia shilingi bilioni 121, sawa na asilimia 10 ya jumla ya fedha zilizokusanywa.
Mchechu amesema ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa mazingira ya biashara pamoja na utekelezaji wa mageuzi mbalimbali ya kiutendaji, kiusimamizi na kiutawala katika mashirika ya umma, hatua ambazo zimeongeza ufanisi na faida za taasisi hizo.


