
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kupungua kwa bei kikomo za mafuta ya petroli nchini kuanzia leo, Julai 1, 2026, baada ya bei za mafuta katika soko la dunia kushuka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA, bei ya petroli imepungua kwa shilingi 96 kwa lita, dizeli kwa shilingi 151 kwa lita, na mafuta ya taa kwa shilingi 242 kwa lita.
Bei kikomo ya lita moja ya petroli katika Jiji la Dar es Salaam sasa ni shilingi 3,990, ikilinganishwa na shilingi 4,086 ya mwezi Juni.
Bei ya dizeli imeshuka kutoka shilingi 4,333 hadi shilingi 4,182 kwa lita, huku mafuta ya taa yakipungua kutoka shilingi 4,685 hadi shilingi 4,443 kwa lita.
EWURA imeeleza kuwa sababu kuu ya kushuka kwa bei hizo ni kupungua kwa bei za mafuta katika soko la kimataifa kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran kuhusu mgogoro wa Mashariki ya Kati.
Makubaliano hayo yameruhusu meli zinazobeba mafuta kuendelea kutumia Mlango wa Bahari wa Hormuz bila vikwazo.
Vilevile, kampuni zinazochakata mafuta ghafi zimeendelea kupata mafuta kutoka maeneo ambayo hayajaathiriwa na vita, hatua iliyosaidia kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa mafuta duniani.
Pamoja na kushuka huko kwa bei, EWURA imebainisha kuwa wastani wa bei za mafuta katika soko la dunia bado haujafikia viwango vilivyokuwepo kabla ya kuanza kwa mgogoro huo mnamo Februari 28, 2026.