
WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amesema Serikali haitaruhusu amani ya nchi ichezewe na akasisitiza kwamba kipaumbele kwa sasa ni usalama wa nchi na raia wake.
“Hatutaruhusu amani ya nchi ichezewe, sisi hatujagusa dola bali tumeshika dola. Kipaumbele chetu kwa sasa ni usalama wa nchi na raia wake,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatano, Julai mosi, 2026) wakati akizungumza na wananchi waliofika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Imbwe, kata ya Kemombo – Nyamongo, wilayani Tarime, mkoani Mara.

Amesema Serikali haitapuuza dalili zozote za fujo na itachukua hatua kali za kisheria. “Hatuwezi kukaa na kuona tunatangaziwa tarehe tu za matukio, tutachukua hatua.”
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Mara, Waziri Mkuu aliendelea kusisitiza suala la amani na umuhimu wa wananchi kutokubali kutumiwa na watu wa nje kuanzisha vurugu nchini.
“Nimekuwa nikisisitiza kwamba amani ya nchi ikivurugwa, muathirika wa kwanza ni mwananchi mwenyewe. Pasiwepo mtu ama kwa makusudi ama kwa kudaganywa wa kukubali kuiwasha moto nchi yako,” amesema na kuongeza kuwa Watanzania wasikubali kufuata mafundisho yanayotolewa mitandaoni kwa lengo la kuanzisha vurugu.