×

Lissu Ataka Kulipwa Fidia Kwa Kudai Kesi Yake Imecheleweshwa Kwa Makusudi

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ameiomba Mahakama ya Rufani ya Dar es Salaam iamuru Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumlipa fidia kwa kile alichodai kuwa ni usumbufu uliotokana na ucheleweshaji wa kesi yake kwa siku 139.

Lissu aliwasilisha ombi hilo mbele ya jopo la majaji watatu, akidai kuwa upande wa Jamhuri umetumia mbinu za kisheria zinazochelewesha mwenendo wa shauri hilo kwa makusudi, hali inayomfanya aendelee kubaki rumande bila sababu za msingi.

Kwa mujibu wa Lissu, ucheleweshaji huo ulianza Februari 24, 2026, na kufikia wakati wa kuwasilisha maombi hayo ulikuwa umefikia siku 139.

Alieleza kuwa tayari ametimiza mwaka mmoja na miezi mitatu tangu alipokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini, akisisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa na upande wa mashtaka zinakiuka haki yake ya kusikilizwa kwa kesi ndani ya muda unaofaa.

Kutokana na hali hiyo, Lissu aliiomba Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya DPP akidai hayana maslahi ya umma, na badala yake iamuru alipwe fidia kwa usumbufu na madhara aliyoyapata kutokana na kucheleweshwa kwa shauri hilo.

Leave a Comment