
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kuwa daraja muhimu la kuwaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara na wanunuzi, huku yakiiunganisha Tanzania na masoko ya kimataifa kwa kipindi cha miaka 50.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Julai 3, 2026, wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), uliofanywa na Rais wa Mozambique, Daniel Chapo, ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi kufuatia mwaliko wa Rais Samia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alisema maonesho hayo yamekuwa chachu ya kukuza biashara na ubunifu, ambapo wabunifu na wajasiriamali wengi walioanza na biashara ndogo wamekua na kufikia viwango vikubwa kupitia fursa zinazotolewa na Sabasaba.

Aliwapongeza waandaaji na washiriki wa maonesho hayo kwa maboresho makubwa yaliyofanyika, hususan katika miundombinu, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa wabunifu ili kuyawezesha maonesho hayo kufikia hadhi kubwa zaidi katika ngazi ya kimataifa.
“Nimefurahi kuona watu tuliokuwa pamoja miaka mingi iliyopita wakati nikiwa ofisa kwenye maonesho haya bado wanaendelea kushiriki na kuchangia maendeleo yake,” alisema Rais Samia.
Alimtaja pia Anna Mkapa, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Equal Opportunity for All Trust Fund (EOTF), kuwa miongoni mwa watu waliodumu katika safari ya maendeleo ya maonesho hayo na walioendelea kushiriki kikamilifu hadi sasa.
Rais Samia alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha Maonesho ya Sabasaba ili yaendelee kuwa jukwaa muhimu la biashara, uwekezaji, ubunifu na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mengine.





