×

Rais Samia na Dk. Mwinyi Kutingisha Kizimkazi Festival 2026

Zanzibar: Kaulimbiu ya “Kizimkazi Kumenoga!” ndiyo inayobeba Tamasha la Kizimkazi 2026, litakalofanyika kuanzia Agosti 12 hadi 14 katika Wilaya ya Kusini Unguja, Zanzibar, likiwa na lengo la kutangaza utalii, uwekezaji, utamaduni pamoja na miradi ya maendeleo.

Tamasha hilo, ambalo limeendelea kujijengea umaarufu kila mwaka, litakuwa na maonyesho ya biashara, burudani, shughuli za kitamaduni na programu mbalimbali zinazolenga kuonesha fursa zilizopo Kizimkazi na Zanzibar kwa ujumla.

Akizungumza Julai 8, 2026 wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya tamasha hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kizimkazi Festival, Mahfodh Said Omar, alisema mwaka huu tamasha limeboreshwa zaidi na kubeba fursa nyingi kwa wawekezaji, wafanyabiashara, wadau wa utalii na wananchi.

Alisema tamasha hilo litafunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Hussein Mwinyi, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga tamasha hilo.

“Tunawaalika wawekezaji, wadau wa maendeleo, wafanyabiashara, wadau wa utalii na wananchi kwa ujumla kushiriki Kizimkazi Festival 2026 kwani mwaka huu tamasha limenoga na limebeba fursa nyingi kwa wote,” alisema Mahfodh.

Alieleza kuwa Kizimkazi Festival ilianzishwa na wazee pamoja na wananchi wa Kizimkazi kwa lengo la kuhifadhi na kuenzi mila, desturi na utamaduni wa eneo hilo, lakini kadri miaka ilivyopita imekua na kuwa jukwaa muhimu la kutangaza utalii, uwekezaji na maendeleo ya jamii.

Miradi ya Maendeleo Kuzinduliwa

Mahfodh alisema tamasha la mwaka huu litaambatana na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa Kizimkazi.

Miradi hiyo ni pamoja na:

  • Uzinduzi wa mradi wa maji wa Kizimkazi.
  • Uzinduzi wa Kiwanja cha Watoto cha Kibuteni.
  • Ufunguzi wa nyumba za makazi za Bopar Enterprises.
  • Uwekaji wa jiwe la msingi la Salaam Cane Restaurant – Kizimkazi Dimbani.
  • Uzinduzi wa mabweni mapya ya Shule ya Sekondari Hasnu Makame – Kibuteni.
  • Uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la maendeleo Kibuteni.
  • Uzinduzi wa Hoteli ya Kitalii ya Johari iliyopo Kizimkazi Mkunguni.

Kutangaza Utalii na Uwekezaji

Kwa mujibu wa waandaaji, tamasha hilo pia litatumika kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii na hoteli, uchumi wa buluu, uvuvi, biashara pamoja na huduma nyingine zinazochangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Mahfodh alisema tamasha hilo linatarajiwa kuongeza idadi ya watalii, kuvutia wawekezaji, kuongeza ajira, kukuza biashara na kuongeza mapato ya wananchi pamoja na Serikali.

Aliongeza kuwa Kizimkazi Festival imekuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Kizimkazi kama eneo lenye historia, vivutio vya utalii na fursa nyingi za uwekezaji kwa manufaa ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Wadau Waalikwa Kushiriki

Waandaaji wamewaalika wawekezaji, wadau wa utalii, kampuni za utalii, waongoza watalii, mashirika ya usafiri, wadhamini, vyombo vya habari, wasanii na wadau wa maendeleo kushiriki tamasha hilo ili kushuhudia fursa zilizopo na kushiriki katika kuitangaza Kizimkazi kimataifa.

“Kizimkazi Festival si tamasha la burudani pekee; ni jukwaa la maendeleo linalounganisha utamaduni, utalii na uwekezaji kwa manufaa ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mahfodh.

Alimalizia kwa kuwakaribisha Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali kuhudhuria tamasha hilo na kushuhudia utajiri wa utamaduni wa Kizimkazi pamoja na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika eneo hilo.

IRAN YATHIBITISHA KUUAWA kwa MWANAJESHI WAKE BAADA ya MASHAMBULIZI MAKUBWA ya MAREKANI….

Leave a Comment