×

Hawajalipwa Fidia, Waapa Kuonana Rais Magufuli

Stori: Makongoro Oging’ UWAZI

Morogoro: Wakulima wa Kata ya Malolo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro ambao mazao yao yaliathiriwa na mpasuko wa bomba la kusafirisha mafuta la Tazama Juni 4,2011 wameapa kumuona Rais John Magufuli ili waweze kulipwa fidia kwani wamekuwa wakiahidiwa kupewa lakini imekuwa ni ahadi hewa.

Baadhi ya wakulima hao Juma Maulid na Mwelesi Ramadhani waliowawakilisha wenzao kuleta kero zao wiki iliyopita katika ofisi ya gazeti hili, wamesema kuwa Rais Magufuli ndiye kimbilio lao kwani hapendi kuona wanyonge wakionewa na serikali yake, wamesema wameandaa timu ya watu sita kwenda ikulu kupeleka malalamiko yao.
Ramadhani amesema mazao yao hasa vitunguu na mahindi yaliharibiwa na mafuta na kuwasababishia umaskini mkubwa lakini serikali iliwaahidi kupitia bungeni chini ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga ambaye kwa sasa ni waziri wa mambo ya ndani, Mei 22,mwaka 2014 kuwa wangelipwa siku chache baada ya kuyaongea bungeni.

Aliendelea kusema kuwa mafuta hayo yaliathiri mazao yao na serikali kupitia bwana shamba wa wilaya alifanya tathmini mwaka huo ambapo waliahidiwa kulipwa mapema lakini hadi leo hakuna kilicholipwa.

“Kwa kweli mafuta hayo yalichafua maji yaliyokuwa yanatumika kwa kunywa na umwagiliaji ambapo wizara ya nishati na madini ilikuwa ikileta maji ya kunywa kwa kutumia magari makubwa kwa muda wa miezi minne lakini hili la kupewa fidia ndiyo imekuwa tatizo, nina wasiwasi huenda fedha hizo zilishatolewa lakini zimetafunwa na wajanja maana hata uongozi wa wilaya ambao ulikuwa ukitutetea kwa karibu kwa sasa hautaki hata kutuona,” alisema mkulima huyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Malolo, Haruna Idd amesema wakulima wa kijiji chake wamepata athari kubwa na kwamba licha ya kufuatilia kulipwa fidia kwa muda mrefu wanazungushwa.
Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ambaye alisema suala hilo wafuatilie Kampuni ya Mafuta ya Tazama.

Leave a Comment