
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi kufuatia Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.
Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu Zanzibar leo, Julai 9, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza maridhiano ya kisiasa, kuimarisha maelewano na kudumisha amani pamoja na utulivu visiwani Zanzibar.
Ajenda zilizotiwa saini zinatarajiwa kuwa msingi wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na pande hizo mbili, zikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kuendeleza maslahi ya wananchi wa Zanzibar.


