×

Makamu wa Rais wa Zambia Anusurika Ajali ya Helikopta ya Jeshi

Makamu wa Rais wa Zambia, Mutale Namulango, amenusurika kifo baada ya Helikopta ya Jeshi la Anga la Zambia (ZAF) aliyokuwa akisafiria pamoja na ujumbe wake kupata ajali katika Mkoa wa Muchinga.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, ndege hiyo ilikuwa ikijaribu kutua ndipo ilipopoteza mwelekeo na kupata ajali muda mfupi baadaye. Picha na video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha ndege hiyo ikiwa imeharibika baada ya tukio hilo.

Serikali ya Zambia imethibitisha kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha katika ajali hiyo, huku Makamu wa Rais na watu wengine waliokuwa ndani ya ndege wakinusurika.

Baada ya ajali, Makamu wa Rais Mutale Namulango alipelekwa katika hospitali iliyo karibu kwa uchunguzi wa afya. Madaktari walibaini kuwa hakuwa na majeraha makubwa na hali yake inaendelea vizuri.

Serikali imewapongeza wananchi wa Mkoa wa Muchinga kwa kutoa msaada wa haraka kwa waathirika wa ajali hiyo, hatua iliyosaidia kuhakikisha wote waliokuwa ndani ya ndege wanapatiwa huduma kwa wakati.

Wakati huo huo, mamlaka husika zimeanzisha uchunguzi rasmi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na hatua zitakazochukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia siku zijazo.

Leave a Comment