
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, maarufu kama MwanaFA usiku wa kuamkia leo Julai 11, 2026 ameshiriki tamasha la kihistoria la kuadhimisha miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo liliwakutanisha wasanii wa vizazi mbalimbali waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji na mafanikio ya muziki wa Bongo Fleva tangu ulipoanza hadi kufikia hatua ya sasa ya kutambulika kimataifa.
Maelfu ya mashabiki waliohudhuria walipata burudani kutoka kwa nyimbo zilizowahi kutamba katika vipindi tofauti, huku kila wimbo ukiamsha kumbukumbu na hisia za safari ndefu ya muziki huo kwa zaidi ya miongo mitatu.

Shamrashamra ziliongezeka pale MwanaFA, ambaye pia ni mmoja wa wasanii walioweka alama katika historia ya Bongo Fleva, alipopanda jukwaani na kuungana na mashabiki kuimba na kucheza baadhi ya nyimbo zilizowahi kufanya vizuri na kuandika historia katika tasnia ya muziki nchini.
Maadhimisho hayo yamekuwa sehemu ya kutambua mchango wa wasanii wa zamani na wa sasa katika kukuza muziki wa Bongo Fleva, ambao umeendelea kuvuka mipaka ya Tanzania na kupata mashabiki katika mataifa mbalimbali duniani.
