
Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kushika kasi baada ya Marekani kutekeleza duru nyingine ya mashambulizi dhidi ya Iran, huku ikisisitiza kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz) unaendelea kuwa wazi kwa meli za biashara licha ya Iran kutangaza kuwa umefungwa.
Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), mashambulizi hayo yalifanyika kufuatia hatua ya Iran kushambulia meli ya mizigo yenye bendera ya Cyprus iliyokuwa ikipita katika njia hiyo muhimu ya kimataifa. Marekani imesema mashambulizi hayo yalilenga kudhoofisha uwezo wa Iran kushambulia usafirishaji wa kimataifa katika eneo hilo.
CENTCOM imeeleza kuwa katika operesheni za mwishoni mwa wiki, jeshi la Marekani lilishambulia zaidi ya malengo 140 ya kijeshi, yakiwemo vituo vya makombora, ndege zisizo na rubani (drones), uwezo wa wanamaji na mifumo ya ulinzi wa pwani. Mashambulizi ya ziada yaliendelea Jumapili yakilenga maeneo mengine ya kijeshi.

Kwa upande wake, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) la Iran lilitangaza kuwa Mlango wa Hormuz umefungwa hadi pale litakapokoma kile lilichokiita “uingiliaji wa Marekani” katika eneo hilo. Pia lilionya kuwa hakuna meli itakayoruhusiwa kupita kwenye njia hiyo hadi taarifa nyingine itakapotolewa.
IRGC ilidai pia kuwa imefanya mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi katika Jordan, Kuwait, Qatar, Oman na Bahrain, huku ikisisitiza kuwa itaendelea kujibu hatua zozote za kijeshi kutoka kwa Marekani na washirika wake.
Hata hivyo, CENTCOM imekanusha madai hayo na kusisitiza kuwa Iran haina mamlaka ya kuufunga Mlango wa Hormuz, ambao unatambulika kimataifa kama njia ya bahari ya kimataifa.
“Iran haidhibiti Mlango wa Hormuz. Njia hiyo inaendelea kuwa wazi, na meli zinaendelea kupita kama kawaida,” ilisema CENTCOM katika taarifa yake.

Mlango wa Hormuz ni moja ya njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa mafuta, ambapo kabla ya vita takriban asilimia 20 ya mafuta yanayouzwa duniani yalikuwa yakipitia katika eneo hilo. Mvutano unaoendelea umeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa usafirishaji wa mafuta na biashara ya kimataifa.
Wakati huo huo, kiongozi mpya wa juu wa Iran, Mojtaba Khamenei, ameapa kulipiza kisasi kufuatia kifo cha baba yake, Ayatollah Ali Khamenei, aliyeuawa katika mashambulizi ya awali ya vita. Amesema Iran itaendelea kupambana hadi waliowajibika wawajibishwe.
Kwa upande mwingine, Rais wa Marekani Donald Trump ameionya Iran dhidi ya jaribio lolote la kuhatarisha maisha yake, akisema Marekani iko tayari kujibu kwa nguvu kubwa endapo tishio lolote litatekelezwa.
Mvutano huo unaendelea kuibua hofu ya kuongezeka kwa mapigano katika Mashariki ya Kati na athari zake kwa uchumi wa dunia, hususan sekta ya nishati na biashara ya kimataifa.