
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeitoza Azam FC faini ya Shilingi milioni 50 kwa kukataa kushiriki sherehe za kukabidhiwa tuzo na zawadi baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB (CRDB Bank Federation Cup 2026).
Adhabu hiyo ilitangazwa leo, Julai 13, 2026, kufuatia kikao cha Kamati ya Mashindano ya TFF kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Azam FC ilikataa kushiriki hafla ya utoaji wa tuzo baada ya kupoteza mchezo wa fainali dhidi ya Simba SC, uliochezwa Julai 4, 2026 katika Uwanja wa Gombani, Pemba. Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, kufuatia bao la kujifunga la kiungo wa Azam FC, Yahya Zeyd.

Mbali na faini hiyo, TFF pia imemfungia kocha wa makipa wa Azam FC, Roudy Mountaro, kwa michezo minne pamoja na kumtoza faini ya Shilingi milioni 2, baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia mwamuzi mara baada ya kumalizika kwa mchezo.
Aidha, mlinda mlango wa Azam FC, Zuberi Foba, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Shilingi milioni 2 kwa kosa la kumshambulia mwamuzi baada ya filimbi ya mwisho.
Wakati huo huo, Jamal Salum Mohamed (Bui) kutoka Azam FC na Ally Mohamed Shatry (Chico) wa Simba SC wamepelekwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya TFF kufuatia vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyodaiwa kutokea baada ya mchezo huo.
Hatua hizo zinaonyesha msimamo wa TFF wa kuhakikisha kanuni na maadili ya mashindano zinazingatiwa, huku ikichukua hatua kali dhidi ya vitendo vinavyokiuka taratibu za soka nchini.
