
Timu ya taifa ya Norway imepokelewa kwa shangwe kubwa na maelfu ya mashabiki jijini Oslo baada ya safari yao ya kihistoria kwenye Kombe la Dunia 2026 kumalizika kwa huzuni katika hatua ya robo fainali.
Zaidi ya mashabiki 100,000 walijaa mitaa ya mji mkuu wa Norway Jumatatu, wakitoa heshima kwa wachezaji wao licha ya kuondolewa kwenye mashindano hayo baada ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya England katika muda wa nyongeza.
Badala ya kuwabeza kutokana na kushindwa kufikia hatua ya nusu fainali, mashabiki waligeuza maumivu hayo kuwa sherehe ya kitaifa, wakisema timu hiyo imeandika historia na kurejesha matumaini ya taifa hilo kwenye soka la dunia.

Kikosi cha Norway kilipowasili Oslo kilipokelewa kwa saluti maalumu ya maji kutoka kwa magari ya zimamoto kabla ya kuanza msafara wa basi la wazi katikati ya jiji.
Maelfu ya mashabiki walikusanyika katika eneo la Ikulu ya Kifalme (Royal Palace), ambapo wachezaji walipata nafasi ya kusalimiana na Mfalme Harald kabla ya kuendelea na sherehe.

Mshambuliaji nyota wa Norway, Erling Haaland, hakushiriki sehemu ya mwisho ya sherehe hizo baada ya kuondoka mapema kutokana na kuchelewa kwa safari kutoka Marekani. Kocha Stale Solbakken alisema Haaland pamoja na Sander Berge walilazimika kuondoka ili kuwahi ndege zao.
Msafara wa timu hiyo ulisababisha msongamano mkubwa katikati ya Oslo, huku polisi wakihangaika kutengeneza njia kutokana na umati mkubwa wa mashabiki waliokuwa wakitaka kuwaona mashujaa wao.

Kulikuwa pia na tukio la kushangaza wakati basi la wazi liliposimamishwa kwa muda baada ya kukutana na nyaya zilizokuwa chini sana. Wachezaji waliokuwa juu ya basi walilazimika kukaa chini ili kuruhusu msafara kuendelea.
Nahodha wa Norway, Martin Ødegaard, amesema sapoti waliyopewa na mashabiki nchini Marekani na nyumbani imekuwa kubwa kuliko walivyotarajia.
“Hatukuwahi kufikiria kupata mapokezi kama haya. Sapoti tuliyoipata imekuwa ya ajabu,” alisema Ødegaard.
Ingawa Norway ilikosa nafasi ya kufika nusu fainali, mafanikio yao kwenye Kombe la Dunia 2026 yameacha alama kubwa katika historia ya soka la taifa hilo.



