×

Airtel Yawapa Vijana Ujuzi wa Kubadili Taka za Kielektroniki kuwa Biashara

Dar es Salaam, Julai 15, 2026 – Airtel Tanzania inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kuwawezesha vijana kwa kuwajengea ujuzi wa kidijitali na teknolojia unaozingatia utunzaji wa mazingira kupitia mafunzo ya urejeshaji na ukarabati wa vifaa vya kielektroniki (e-waste). Mafunzo hayo yalitolewa wakati wa warsha ya ReFab Dar 2, iliyofanyika jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana na Stadi 2026.

Warsha hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), BUNI Hub, Airtel Fursa Lab, na TechStar Innovation Hub, wenye kauli mbiu isemayo “Kubadili Taka za Kielektroniki kuwa Fursa kupitia Ujuzi, Ubunifu na Uchumi wa Mzunguko.”

Ambapo jukwaa hilo liliwakutanisha wanafunzi wa vyuo vikuu, vyuo vya ufundi stadi (TVET), wahitimu wa TEHAMA, wajasiriamali na wabunifu chipukizi ili kupata mafunzo ya vitendo kuhusu ukarabati wa vifaa vya kielektroniki, usimamizi wa taka za kielektroniki na mbinu salama za urejelezaji.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Bi. Beatrice Singano, alisema kuwa moja ya misingi muhimu ya kujenga uchumi endelevu wa kidijitali nchini ni kuwawezesha vijana kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo unaowawezesha kutumia teknolojia kwa ubunifu huku wakizingatia utunzaji wa mazingira.

“Tunaamini kuwa uwekezaji wenye tija zaidi kwa taifa ni ule unaowawezesha vijana wake. Kupitia teknolojia, ujuzi wa vitendo na ubunifu, tunawapa vijana uwezo wa kujiajiri, kutatua changamoto za jamii, kuchangia maendeleo ya taifa na kulinda mazingira yanayotuzunguka,” alisema Bi. Singano.

Katika kuendeleza juhudi hizo, Airtel Tanzania imekabidhi jumla ya kompyuta 35 kwa DTBi kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya vitendo. Programu zinazotolewa kwa sasa ni pamoja na uandishi wa programu (coding), ukarabati wa kompyuta, utafiti, pamoja na kukuza ubunifu na ujasiriamali kwa vijana.

Kupitia ushirikiano kati ya Airtel Tanzania na DTBi chini ya mradi wa Airtel Fursa Lab, vijana na wanawake wanaendelea kunufaika na mafunzo ya ujuzi wa kidijitali, elimu ya ujasiriamali na uchumi. Hadi sasa, zaidi ya vijana na wajasiriamali 5,300 wamenufaika kupitia vituo vinne vya ubunifu vilivyopo Dar es Salaam na Zanzibar.

Bi. Singano alisema ushirikiano huo kati ya sekta binafsi na wadau wa maendeleo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuwajengea vijana uwezo unaohitajika ili kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi endelevu wa kidijitali.

“Tunataka vijana waache kuona taka za vifaa vya kielektroniki kama taka zisizo na thamani, bali wazione kama fursa. Kompyuta inayokarabatiwa leo inaweza kuwa nyenzo ya kujifunzia kesho, na ujuzi wanaoupata leo unaweza kuwa msingi wa biashara yenye mafanikio katika sekta ya teknolojia ya kijani,” alisema.

Airtel Tanzania pia inaendelea kuwa mstari wa mbele kupitia mradi wa E-Waste Go Green, unaohamasisha usimamizi salama wa taka za vifaa vya kielektroniki kupitia elimu, ukusanyaji na urejelezaji salama wa taka hizo.

Zaidi ya asilimia 50 ya minara ya mawasiliano ya Airtel Tanzania sasa imeunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa, hatua inayoongeza matumizi ya nishati safi, kuboresha ufanisi wa huduma na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2025/26, Airtel Africa katika nchi 14, ikiwemo Tanzania, iliokoa zaidi ya lita milioni 9.1 za dizeli, huku asilimia 94 ya taka zote zilizozalishwa katika shughuli zake zikirejelewa, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuendeleza uwajibikaji wa mazingira na maendeleo endelevu.

Leave a Comment