
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemsimamisha kufanya shughuli zote za chama aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Roman Selasini, huku kikimpa siku 14 za kujieleza kwa maandishi kuhusu sababu ambazo zingezuia kuchukuliwa hatua kali zaidi za kinidhamu dhidi yake kutokana na tuhuma za ukiukaji wa maadili ya chama.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kikao cha dharura cha CHADEMA Kata ya Makiidi kilichofanyika Julai 14, 2026, ambacho kilijadili mwenendo wa mwanasiasa huyo anayeshutumiwa kutumia vyombo vya habari kutoa matamko na shutuma dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, badala ya kutumia mifumo rasmi ya chama kushughulikia malalamiko yake.
Kupitia barua rasmi iliyotolewa Julai 15, 2026, uongozi wa chama hicho umeeleza kuwa Selasini, ambaye ni mwanachama mwenye kadi namba CDM 496369, amezuiwa kushiriki shughuli zote za uongozi na utendaji wa chama kuanzia mara moja.
“Kuanzia tarehe ya kupokea barua hii, huruhusiwi kushiriki kuongoza wala kutekeleza shughuli zozote za chama hadi utakapokamilisha utaratibu wa kujieleza na shauri lako litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Chama,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo imefafanua kuwa kitendo cha kutoa shutuma hadharani dhidi ya viongozi wakuu wa chama ni ukiukaji wa wazi wa Ibara ya 10.1(iv) na 10.1(v) ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006 (Toleo la 2019).
Selasini anapaswa kuwasilisha utetezi wake wa maandishi ndani ya siku 14 kwa mujibu wa Ibara ya 63.6(c) ya Katiba ya chama, hatua ambayo inaweza kuamua hatma yake ndani ya CHADEMA, ikiwemo uwezekano wa kuchukuliwa hatua kali zaidi za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufukuzwa uanachama.