×

Mzamiru Yassin Aaga Rasmi Simba Baada ya Miaka Tisa ya Utumishi

Klabu ya Simba SC imethibitisha rasmi kuachana na kiungo wake mkongwe Mzamiru Yassin, baada ya mkataba wake kumalizika, ikiwa ni sehemu ya mabadiliko ya kikosi kuelekea msimu wa mashindano wa 2026/27.

Mzamiru, ambaye ameihudumia Simba kwa takribani miaka tisa, anaondoka akiwa mmoja wa wachezaji walioacha alama ndani ya kikosi hicho kutokana na mchango wake katika mafanikio mbalimbali ya klabu ndani na nje ya nchi.

Kwa kuondoka kwake, Mzamiru anakuwa mchezaji wa nane kupewa mkono wa kwaheri na Wekundu wa Msimbazi katika dirisha hili la usajili. Wengine waliotanguliwa kuondoka ni Moussa ‘Pin Pin’ Camara, Joshua Mutale, Naby Camara, Chamou Karaboue, Awesu Awesu, Edwin Balua na Omari Omari.

Taarifa zinaeleza kuwa kiungo huyo tayari amekamilisha usajili wake katika TRA United, akitia saini mkataba wa miaka miwili baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa mkopo msimu uliopita.

Kuondoka kwa Mzamiru ni sehemu ya mkakati wa Simba wa kufanya maboresho ya kikosi chake, huku klabu ikiendelea kusajili wachezaji wapya kwa lengo la kuunda timu imara itakayowania mataji katika msimu ujao.

Leave a Comment