×

Wachezaji wa Uingereza Waanza Kumlalamikia Kocha Baada ya Kuondolewa na Argentina

Wachezaji kadhaa wa timu ya taifa ya England (Uingereza) wameelezwa kutoridhishwa na namna timu hiyo ilivyocheza katika dakika za mwisho za mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Argentina.

England ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Argentina baada ya kuongoza kwa muda mrefu, lakini ikaanguka katika dakika za mwisho kutokana na presha kubwa kutoka kwa mabingwa hao wa dunia.

Baadhi ya wachezaji wakubwa ndani ya kikosi hicho waliamini timu ilirudi nyuma mapema mno baada ya kupata bao la kuongoza, jambo lililowapa Argentina nafasi ya kutawala mchezo.

Kocha mkuu wa England, Thomas Tuchel, aliweka mfumo wa ulinzi wa watu watano (back five) katika kipindi cha mwisho cha mchezo ili kulinda matokeo, lakini hatua hiyo imezua mjadala mkubwa.

Baadhi ya wachezaji wanaamini England ilipaswa kuendelea kusukuma mbele na kuwazuia Argentina kwa kuwapa presha badala ya kuruhusu wapinzani wao kumiliki mpira na kushambulia mfululizo.

Mmoja wa watu wa karibu na timu hiyo alinukuliwa akisema:

“Walirudi nyuma sana mapema mno.”

Hata hivyo, Tuchel amekanusha kuwa mpango wake ulikuwa timu ishuke nyuma, akisema walishindwa kupata ushindi wa mipira ya duwa na hivyo kulazimika kurudi nyuma.

“Haikuwa mpango kushuka zaidi na zaidi. Tulihitaji kurudi kwenye mpira, kwa sababu bila kufanya hivyo huwezi kuvunja presha na kurejesha nguvu ya mchezo,” alisema Tuchel.

Kocha huyo pia aligusia changamoto ya kiutamaduni katika mtindo wa soka wa England akisema tofauti na mataifa kama Hispania, Argentina na Brazil, timu yao bado inahitaji kuboresha uwezo wa kumiliki mpira na kudhibiti mchezo.

Licha ya kufika hatua ya nusu fainali, England sasa inakabiliwa na tathmini kubwa kuhusu mbinu na mustakabali wa Tuchel, ambaye aliteuliwa kwa matumaini ya kuifanya timu hiyo kuvunja ukame wa mataji tangu mwaka 1966.

Leave a Comment