×

Trump Kuhudhuria Fainali ya Kombe la Dunia 2026 Kwa Mara ya Kwanza

Rais wa Marekani Donald Trump atahudhuria fainali ya Kombe la Dunia 2026 itakayowakutanisha Hispania na Argentina siku ya Jumapili, Ikulu ya Marekani imethibitisha.

Hii itakuwa mara yake ya kwanza kuonekana kwenye michuano hiyo tangu ilipoanza, huku akitarajiwa kuwa sehemu ya hafla kubwa ya kufunga mashindano hayo na kumkabidhi kombe mshindi wa fainali itakayochezwa New Jersey.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt, amesema uwepo wa Trump utakuwa hitimisho la mashindano ambayo yameelezwa kuwa miongoni mwa yaliyotazamwa zaidi na yenye ulinzi mkubwa katika historia ya Marekani.

“Ushiriki wake utahitimisha Kombe la Dunia lililokuwa na mafanikio makubwa na kuonyesha uwezo wa Marekani kuikaribisha dunia kwenye jukwaa kubwa zaidi,” alisema Leavitt.

Mbali na fainali hiyo, Trump pia atahudhuria mapokezi ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) yatakayofanyika katika jengo lake la Trump Tower jijini New York.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alikuwa ametangaza mwezi Juni kuwa Trump angehudhuria fainali na kukabidhi kombe kwa mabingwa, lakini uthibitisho rasmi ulikuwa unasubiriwa kutoka Ikulu ya Marekani.

Hata hivyo, Leavitt amesema hajui ni timu gani Trump ataipa sapoti kati ya Argentina na Hispania, hasa baada ya rais huyo kumkosoa Hispania katika mkutano wa NATO kutokana na msimamo wake kuhusu vita vya Iran.

Ingawa Trump hajahudhuria mchezo wowote wa Kombe la Dunia hadi sasa, amekuwa akihusishwa na michuano hiyo baada ya kuingilia suala la mchezaji wa Marekani Folarin Balogun, ambaye alipata adhabu ya kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Bosnia.

Trump alisema alimwomba Infantino kupitia upya uamuzi huo, na FIFA baadaye ikasimamisha adhabu ya mechi moja kwa Balogun kabla ya mchezo wa Marekani dhidi ya Ubelgiji.

Trump pia amekuwa akidai kuwa alisaidia kuhakikisha Marekani inapata nafasi ya kuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Dunia 2026 pamoja na Canada na Mexico, uamuzi uliotolewa wakati wa kipindi chake cha kwanza madarakani.

Uhusiano wa karibu kati ya Trump na Infantino umeonekana katika miaka ya hivi karibuni, huku rais huyo wa FIFA akimpa Trump tuzo maalumu ya amani ya FIFA wakati wa droo ya Kombe la Dunia.

Uamuzi wa Trump kukabidhi kombe la dunia unakumbusha tukio la mwaka uliopita kwenye Fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu, ambapo alimkabidhi nahodha wa Chelsea, Reece James, kombe baada ya ushindi dhidi ya Paris Saint-Germain, lakini alibaki jukwaani wakati wa shangwe za wachezaji na kusababisha mshangao.

Leave a Comment