
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kesho Julai 18, 2026 kwa ziara ya kitaifa yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kihistoria na ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Misri.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu leo Julai 17, 2026, wakati wa ziara hiyo Rais El-Sisi atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mazungumzo ya viongozi hao yanatarajiwa kujikita katika namna ya kuongeza nguvu ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali muhimu, ikiwemo biashara, uwekezaji, kilimo, nishati, maji, afya, elimu pamoja na miundombinu.

Mbali na mazungumzo ya viongozi hao wawili, Rais Samia na Rais El-Sisi pia wanatarajiwa kushiriki katika Jukwaa la Biashara la Tanzania na Misri, litakalowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi hizo mbili.
Jukwaa hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya kujadili fursa mpya za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi, huku Tanzania na Misri zikiendelea kutafuta njia za kuongeza manufaa kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.
Kwa muda mrefu, Tanzania na Misri zimekuwa na uhusiano wa karibu katika nyanja mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo, mafunzo ya wataalamu, kubadilishana uzoefu na ushirikiano katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ziara ya Rais El-Sisi inatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuendeleza uhusiano huo na kufungua fursa mpya za ushirikiano wenye tija kwa wananchi wa Tanzania na Misri.
