
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hatakamatwa akiwa nchini Marekani licha ya kuwepo kwa hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Trump alitoa kauli hiyo kupitia mtandao wake wa Truth Social, akisema, “Benjamin Netanyahu hatakamatwa kwa namna yoyote ile akiwa ndani ya Marekani.” Hata hivyo, hakumtaja moja kwa moja Meya wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, ambaye hivi karibuni alisema mamlaka ya jiji hilo zinaendelea kuchunguza hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa iwapo Netanyahu atawasili.
Katika ujumbe wake, Trump pia aliisifu Israel kwa mchango wake katika vita dhidi ya Iran.
Kwa upande wake, Mamdani alisema katika mahojiano na The New York Times kuwa anaamini Netanyahu anapaswa kufikishwa mjini The Hague, akimtaja kuwa mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita kulingana na mashtaka yaliyowasilishwa na ICC.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu ikimtuhumu kwa madai ya uhalifu wa kivita unaodaiwa kutendwa wakati wa vita vya Gaza. Hata hivyo, Israel imekataa mamlaka ya mahakama hiyo na imeendelea kupinga tuhuma hizo, ikisisitiza kuwa haijafanya uhalifu wa kivita.
Netanyahu kwa kawaida hutembelea New York mwezi Septemba kila mwaka kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).