
Mzee mwenye umri wa miaka 65, Carl Isom-McDaniel, amezungumza akiwa hospitalini baada ya kushambuliwa na mnyama aina ya bison (ni mnyama mkubwa jamii ya ng’ombe pori lakini ana mwili mkubwa zaidi na uzito wa Tani Moja) katika Hifadhi ya Taifa ya Yellowstone nchini Marekani, ambapo alirushwa hewani na kuvunjika mfupa mkubwa wa paja katika sehemu nne.

Tukio hilo lilitokea wakati Carl alipokuwa akitembea na mjukuu wake katika eneo la hifadhi hiyo. Bison huyo mwenye uzito wa takribani tani moja alionekana kukasirika na kumfuata kwa kasi kabla ya kumshambulia na kumrusha umbali wa futi nane angani.
Vipimo vya X-ray vilionyesha kuwa mfupa wake wa paja (femur) ulivunjika katika maeneo manne karibu na nyonga, jeraha ambalo daktari wake alilitaja kuwa ni la maumivu makubwa.

Akizungumza akiwa hospitalini, Carl alisema awali bison huyo hakuonekana kuwa na dalili za ukali, lakini ghafla alichagua kumshambulia.
“Nilikuwa na mjukuu wangu wakati huo. Nilijaribu kukimbia, lakini aliendelea kunifuata. Aliponifikia alinirusha hewani. Sikupata majeraha makubwa wakati wa kurushwa, tatizo lilikuwa nilipotua chini,” alisema.

Carl alisema anashukuru kunusurika kifo, akiamini hali ingeweza kuwa mbaya zaidi.
Mpiga picha wa kitaalamu, Mike MacLeod, aliyenasa tukio hilo kwa kamera, alisema Carl alikuwa na maumivu makali lakini bado alikuwa na fahamu na hata alikuwa akitania baada ya tukio.
Hifadhi ya Taifa ya Yellowstone ilithibitisha kuwa tukio hilo lilitokea Julai 10 katika eneo la Bridge Bay Campground karibu na Ziwa Yellowstone, ambapo wahudumu wa dharura walimsaidia na kumpeleka hospitalini.


TRUMP ALIPUKA MASHAMBULIZI ya IRAN KUUA WANAJESHI 3 wa MAREKANI – ASEMA IRAN ITALIPA GHARAMA KUBWA..