×

Jurgen Klopp Ateuliwa Kuwa Kocha Mpya Wa Timu Ya Taifa Ya Ujerumani

Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB) limemtangaza rasmi Jurgen Klopp kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo, akipewa jukumu la kuijenga upya timu hiyo iliyopitia kipindi kigumu katika miaka ya hivi karibuni.

Klopp, aliyewahi kuinoa Liverpool na kushinda mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, amesaini mkataba utakaomuweka kwenye nafasi hiyo hadi mwaka 2030, ukiwahusisha pia maandalizi ya Kombe la Dunia la 2030 litakalofanyika Hispania, Ureno na Morocco.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 amechukua nafasi ya Julian Nagelsmann, aliyeondoka baada ya Ujerumani kutolewa mapema kwenye Kombe la Dunia baada ya kufungwa na Paraguay katika hatua ya 32 bora kwa mikwaju ya penalti.

Akizungumza baada ya kutangazwa rasmi mjini Frankfurt, Klopp amesema ni heshima kubwa kwake kupewa nafasi hiyo na ameahidi kutoa kila alichonacho kuirudisha Ujerumani katika kiwango chake cha zamani.

“Hii ni heshima kubwa kwangu. Nitatoa kila kitu nilichonacho,” amesema Klopp.

Hata hivyo, Klopp ameonya kuwa hatavumilia mazingira mabaya ya kazi, akisema endapo mashabiki au vyombo vya habari vitaanza kumdharau bila sababu, yuko tayari kuondoka.

Tangu mwaka 2025, Klopp alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Red Bull kama Mkuu wa Soka Duniani, akisimamia klabu zinazomilikiwa na kampuni hiyo ikiwemo RB Leipzig, Red Bull Salzburg na New York Red Bulls.

DFB imesema haitalipa ada ya kuvunja mkataba wake na Red Bull, badala yake itatoa mchango wa euro milioni moja kwa taasisi ya Wings for Life, inayofanya utafiti wa majeraha ya uti wa mgongo.

Klopp anakabiliwa na kazi kubwa ya kuirejesha Ujerumani kwenye kilele cha soka la dunia baada ya kushindwa kufanya vizuri katika mashindano makubwa ya hivi karibuni.

Ujerumani imeshindwa kuvuka hatua za juu kwenye Kombe la Dunia mara tatu mfululizo tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 2014.

Kocha huyo anatarajiwa kujenga timu yake akiwategemea nyota chipukizi kama Florian Wirtz na Jamal Musiala, huku akishirikiana na mkurugenzi wa michezo Rudi Völler.

Mechi yake ya kwanza inatarajiwa kuwa katika Ligi ya Mataifa dhidi ya Uholanzi Septemba 24, 2026.

Leave a Comment