
Maafisa wa usafirishaji pamoja na vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu katika Jimbo la Buchosa wanaendelea kunufaika na mafunzo ya elimu ya fedha yanayotolewa na CRDB Foundation kupitia programu ya Imbeju, inayolenga kuwawezesha kupata mikopo ya pikipiki kutoka Benki ya CRDB.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kifedha na kuwapa uelewa wa namna bora ya kutumia mikopo hiyo ili kuanzisha au kukuza shughuli za kiuchumi zinazoweza kuboresha maisha yao.

Fursa hiyo imewezeshwa na Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, ambaye ameendelea kusukuma jitihada za kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kupitia programu mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa wa CRDB Foundation, Ephraim Kalambo, kwa kushirikiana na Isack Ibrahimu, aliwataka wanufaika watakaopata mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili iwe chachu ya maendeleo yao binafsi, familia zao na jamii kwa ujumla.
Maafisa hao walisisitiza kuwa matumizi sahihi ya mikopo yatawawezesha wananchi kuongeza kipato, kuimarisha biashara zao na kujenga msingi imara wa maendeleo endelevu.
