
Washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal ya Fasihi ya Afrika wametangazwa rasmi katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, huku waandishi wa Tanzania wakiibuka washindi katika sehemu kubwa ya tuzo hizo zinazolenga kukuza na kuendeleza fasihi ya Kiswahili barani Afrika.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliyewakilishwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Riziki Pembe.
Katika hotuba yake, Waziri Makonda aliipongeza Safal Group kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills ya Kenya na ALAF Limited ya Tanzania kwa kuendelea kudhamini tuzo hizo kwa kipindi cha miaka 10, akieleza kuwa mchango huo umeendelea kuikuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Afrika.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kuimarisha matumizi ya Kiswahili na kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kutambulika duniani. Pia aliwataka washindi kutumia vipaji vyao kuendelea kuandika kazi zenye ubora na kuzigeuza kuwa chanzo cha kipato kupitia uchapishaji na mauzo ya vitabu.
Katika matokeo yaliyotangazwa, Salim Hussein Ng’azi wa Tanzania alishinda nafasi ya kwanza katika kipengele cha riwaya kupitia kazi yake Mwanamkasi Ndio Basi na kujinyakulia dola 5,000 za Marekani, huku Dickson Damas Mtalaze akishika nafasi ya pili kwa riwaya Shamba la Mawe na kujishindia dola 2,500.
Kwa upande wa ushairi, Ali Hilal Ali alitwaa ushindi wa kwanza kupitia Diwani ya Vizikwa ya Kale na kujishindia dola 5,000, wakati Leonard Barnaba Mtesigwa alimaliza katika nafasi ya pili kwa Rima la Miiko la Balaa na kupata dola 2,500.

Katika kipengele cha hadithi fupi, Dominic Maina Oigo kutoka Kenya aliibuka mshindi kupitia kazi yake Mbunge Mtarajiwa na Hadithi Nyingine na kujishindia dola 2,500.
Waandaaji wa tuzo hizo walisema jumla ya miswada 230 kutoka mataifa saba ya Afrika iliwasilishwa mwaka huu, hali iliyoonyesha kuongezeka kwa ushindani na ubora wa kazi za fasihi ya Kiswahili.
Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Bibhu Nanda, alisema kampuni hiyo imeendelea kudhamini tuzo hizo kutokana na mchango mkubwa wa lugha ya Kiswahili katika kuunganisha watu wa Afrika Mashariki na kurahisisha biashara katika ukanda huo.
Kwa upande wake, mmoja wa waanzilishi wa tuzo hiyo, Dkt. Lizzy Attree, alisema katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, tuzo hiyo imeshatoa zaidi ya dola 150,000 kwa waandishi zaidi ya 40 na kusaidia kuchapishwa kwa zaidi ya vitabu 20.
Mwenyekiti wa jopo la majaji, Profesa Rayya Timammy wa Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema ushindani wa mwaka huu ulikuwa mkubwa kutokana na ubora wa kazi zilizowasilishwa, jambo linaloonyesha kuwa fasihi ya Kiswahili inaendelea kukua na kupata waandishi wenye vipaji vya hali ya juu.
Mbali na zawadi za fedha, kazi zilizoshinda zitachapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota, huku diwani ya mashairi iliyoshinda ikitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kuchapishwa na African Poetry Book Fund (APBF), hatua inayotarajiwa kuendelea kuitangaza fasihi ya Kiswahili katika jukwaa la kimataifa.