
Mwanamke mwenye umri wa miaka 32 nchini Marekani amefunguliwa mashtaka ya mauaji baada ya kudaiwa kumuua baba yake katika nyumba waliyokuwa wakiishi pamoja katika eneo la Morgan Township, jimbo la Indiana.
Mshukiwa huyo ametajwa kuwa Serena Desiree Dolnics, ambaye anadaiwa kumuua baba yake, Gregory Dolnics, kabla ya kukamatwa na polisi baada ya kufanyika ukaguzi wa usalama kufuatia taarifa za familia kuwa walikuwa hawajapata mawasiliano naye kwa muda.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, ndugu wa Gregory walianza kuwa na wasiwasi baada ya simu zao kutopokelewa. Familia hiyo ilidai kuwa Serena alikuwa akitoa kauli zisizo za kawaida walipokuwa wakitaka kuzungumza na baba yake.
Inadaiwa kuwa kabla polisi hawajafika eneo la tukio, mpenzi wa Serena aliwasiliana na familia hiyo na kueleza kuwa alimwona akiwa na damu mwilini, jambo lililomfanya kuwa na hofu kuhusu hali iliyokuwa ikiendelea ndani ya nyumba hiyo.
Polisi walipofika walimkuta Gregory akiwa amefariki ndani ya nyumba hiyo na baadaye Serena akachukuliwa kuwa mshukiwa mkuu wa tukio hilo.
Hadi sasa, mamlaka za Marekani hazijatoa sababu rasmi iliyosababisha tukio hilo, na nyaraka za mahakama hazijaonyesha wazi chanzo cha ugomvi au mazingira yaliyosababisha kifo cha Gregory.
Wapelelezi bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kilichopelekea tukio hilo, huku Serena akikabiliwa na shtaka moja la mauaji.
Katika mahojiano ya awali na polisi, Serena alidai kuwa yeye na baba yake walikuwa wanaelewana vizuri na hakukuwa na tatizo lolote kati yao.
Serena alifikishwa mahakamani na kukana mashtaka yanayomkabili. Kwa sasa anazuiliwa bila dhamana huku mchakato wa kisheria ukiendelea.