×

Exim na YST Waendeleza Uwekezaji kwa Vijana Wabunifu kwa Mwaka wa Sita Mfululizo

Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza (kushoto), akisalimiana na Mwanzilishi Mwenza wa Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), Dkt. Gozibert Kamugisha (kulia).

Dar es Salaam Tanzania, 31 Julai 2026: Benki ya Exim Tanzania na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) leo wamezindua rasmi ushirikiano wao wa mwaka 2026 kupitia Programu ya YST 2026, wakithibitisha dhamira yao ya pamoja ya kuendelea kuandaa kizazi kijacho cha wabunifu, watafiti na watatuzi wa changamoto kupitia sayansi, teknolojia, ubunifu na utafiti.

Ushirikiano huu unafikisha mwaka wa sita mfululizo tangu Benki ya Exim Tanzania ilipoanza kuunga mkono Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), jambo linalodhihirisha dhamira ya Benki ya kuwekeza katika elimu, ubunifu na maendeleo ya vijana, huku ikichangia maendeleo ya muda mrefu ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya Exim Tanzania (Exim Tower) jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, alisema ushirikiano huo unaakisi imani ya Benki kuwa kuwawezesha vijana ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye ubunifu, ushindani na maendeleo endelevu kupitia falsafa yao ya “Ubunifu ni maisha”.

“Exim Bank Tanzania tunaamini kuwa ubunifu huanza kwa kuwawezesha vijana. Ushirikiano wetu na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) unaonesha dhamira yetu ya kuwaunga mkono wanafunzi wenye udadisi, ubunifu na ari ya kutafuta suluhisho zinazoweza kubadilisha jamii na kuchangia maendeleo ya taifa”. alisema D’Souza.

“Kwa miaka sita sasa, YST imekuwa mshirika wetu muhimu katika kuwaibua na kuwawezesha vijana wenye fikra bunifu kutumia sayansi, utafiti na ubunifu kutatua changamoto zinazoikabili jamii. Tunaamini kuwa kwa kuwekeza katika elimu, ubunifu na maendeleo ya vipaji vya vijana leo, tunajenga msingi imara wa maendeleo endelevu ya Tanzania”. Aliongeza D’Souza

Programu ya mwaka huu imeweka rekodi mpya kwa kupokea jumla ya mawasilisho 1,330 ya miradi kutoka shule 287 za sekondari zilizopo katika mikoa yote ya Tanzania. Baada ya mchakato wa tathmini na ulezi wa kitaalamu uliofanywa na washauri wa sayansi wa YST, miradi 162 imechaguliwa kuingia hatua inayofuata, huku miradi 45 bora ikitarajiwa kushiriki Maonesho ya Kitaifa ya Sayansi na Teknolojia ya taasisi ya wanasayansi chipukizi yatakayofanyika tarehe 17 Septemba 2026 katika Ukumbi wa maktaba mpya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumzia ushirikiano huo, Mwanzilishi Mwenza wa taasisi ya wanasayansi chipukizi Tanzania, Dkt. Gozbert Kamugisha, aliishukuru Benki ya Exim Tanzania kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu katika kuwawezesha vijana wabunifu nchini.

“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Benki ya Exim Tanzania kwa msaada wake endelevu katika kipindi cha miaka sita iliyopita.Kilichoifanya programu ya mwaka huu kuwa ya kipekee ni kwamba Benki ya Exim Tanzania haijajikita tu katika kutoa udhamini wa kifedha, bali pia imekuwa sehemu ya utekelezaji wa programu. Kupitia wataalamu wake, Benki imeungana nasi kutembelea shule mbalimbali, kukutana na walimu na wanafunzi, pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu unaowasaidia kuboresha tafiti na ubunifu wao ili kupata suluhisho zenye tija kwa jamii,” aliongeza Dkt. Kamugisha

Katika hatua nyingine, Dkt. Gozibert Kamugisha alibainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili YST, ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha unaozuia kuwafikia vijana wote wenye vipaji na mawazo bunifu, pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika maendeleo ya vijana wabunifu.

“Bado jamii haijaelewa vya kutosha kwamba kama taifa hatuwezi kufikia maendeleo tunayoyataka bila kuwekeza kwa dhati katika vijana wetu, hususan katika sayansi, teknolojia na ubunifu. Tukitazama mataifa yaliyopiga hatua, yamewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuwawezesha vijana kufanya utafiti, ubunifu na ugunduzi. Serikali imeweka sera na mazingira mazuri ya kuhamasisha ubunifu, sasa ni wajibu wetu kuungana na kuhakikisha vijana wetu wanapata fursa za kutimiza ndoto zao na kuchangia maendeleo ya Taifa.” Aliongeza Kamugisha

Kwa zaidi ya miaka 16, taasisi ya wanasayansi chipukizi Tanzania (YST) imekuwa ikiwajengea uwezo wanafunzi wa shule za sekondari katika utafiti wa kisayansi na ubunifu kupitia programu za mafunzo na uhamasishaji, zikiwawezesha kutambua changamoto zinazozikabili jamii na kubuni suluhisho zinazotekelezeka na zenye kuendana na mazingira ya Tanzania.

Ushirikiano wa Exim Bank unaimarisha dhamira hiyo kwa kuwaunga mkono vijana wanaobuni suluhisho katika maeneo mbalimbali, ikiwemo akili unde (Artificial Intelligence), kilimo na mifugo, uhifadhi wa mazingira, afya, usalama wa chakula, mawasiliano na ubunifu wa kijamii.

Ikiongozwa na falsafa yake ya “Ubunifu ni maisha”, benki ya Exim Tanzania inaendelea kuunga mkono mipango inayofungua fursa kwa vijana wa Kitanzania na kuhamasisha ubunifu wa ndani. Kupitia ushirikiano wa kimkakati na YST, kwa zaidi ya miaka sita sasa toka mwaka 2021, Benki hiyo inaendelea kuwasaidia vijana kutumia elimu na maarifa wanayopata darasani kubuni suluhisho za changamoto halisi zinazoikabili jamii, huku ikikuza utamaduni wa utafiti, ubunifu, ujasiriamali na maendeleo ya teknolojia.

Wakati maandalizi ya Maonesho ya Kitaifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2026 yakiendelea, Benki ya Exim Tanzania na Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) wanaendelea kushirikiana kuwawezesha vijana wabunifu ambao mawazo, tafiti na ugunduzi wao vitachangia kujenga Tanzania yenye ubunifu zaidi, ushirikishwaji na ustawi endelevu.

Leave a Comment