×

FIFA Yatoa Siku 53 kwa Wanachama Kuamua Hatima ya Hisa za Kombe la Dunia

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amezipa nchi zote wanachama 211 wa shirikisho hilo zikiwemo nchi 54 za Afrika — siku 53 kuamua kama zitaunga mkono mpango wenye utata wa kuuza sehemu ya hisa za haki za kibiashara za Kombe la Dunia, au zikubali kupoteza sehemu kubwa ya fedha za maendeleo zinazotolewa na FIFA.

Kupitia barua aliyowatumia viongozi wa mashirikisho yote ya soka duniani, Infantino ameweka tarehe 19 Septemba kuwa mwisho wa kutoa uamuzi kuhusu pendekezo la kuuza kati ya asilimia 20 hadi 30 ya haki za kibiashara za FIFA kwa wawekezaji binafsi.

Mashirikisho yatakayokubali mpango huo yanatarajiwa kunufaika na mfuko wenye thamani ya hadi dola bilioni 10, ambapo kila shirikisho linaweza kupata hadi dola milioni 40.

Hata hivyo, mashirikisho yatakayoukataa mpango huo yatapata takribani dola milioni 10 pekee katika kipindi cha miaka minne ijayo, jambo linalomaanisha kupoteza karibu dola milioni 30, sawa na takribani asilimia 75 ya fedha zilizokuwa zikitarajiwa.

Kwa mashirikisho mengi ya soka barani Afrika, suala hili lina uzito mkubwa kutokana na utegemezi wao wa fedha za FIFA katika kuendesha shughuli za maendeleo ya soka.

Mpango huo, ambao unadaiwa kuhusishwa na wawekezaji wenye ukaribu na duru za Rais wa Marekani, Donald Trump, umekosolewa vikali na UEFA, ambayo imesisitiza kuwa Kombe la Dunia si “rasilimali ya biashara inayoweza kuuzwa.”

Licha ya upinzani huo, Confederation of African Football imeendelea kuwa mshirika mkubwa wa Infantino na tayari imetangaza kumuunga mkono katika azma yake ya kugombea tena urais wa FIFA mwaka 2027.

Leave a Comment