
Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, ameshiriki picha akiwa pamoja na mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji (MO) wakati wa ziara yake ya mapumziko mjini Dubai, akieleza kufurahishwa na mazungumzo waliyofanya kuhusu maendeleo ya Tanzania.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Shigongo amesema yupo Dubai kwa mapumziko mafupi akiwa na familia yake, ambapo walipata heshima ya kualikwa nyumbani kwa Mohamed Dewji.

Ameeleza kuwa walijadili masuala mbalimbali ikiwemo maendeleo ya nchi, imani kwa Mungu na namna bora ya kuwasaidia Watanzania kujikwamua kutoka kwenye umasikini kwa kutumia vipawa, maarifa na rasilimali walizojaliwa.
Shigongo amesema siku hiyo ilikuwa ya furaha na baraka nyingi, huku akimsifu Mohamed Dewji kuwa ni mtu mwema, mnyenyekevu, mwenye hofu ya Mungu na mwenye moyo wa kuwajali wengine.

“MO ni mtu mwema, mnyenyekevu, mwenye hofu ya Mungu na mwenye moyo wa kuwajali wengine. Kwa sifa hizo, naweza kumtetea popote,” ameandika Shigongo, akihitimisha kwa kumtakia baraka zaidi kutoka kwa Mungu.
