
Wamiliki wa vituo vya kulelea watoto nchini wametakiwa kuwekeza katika mafunzo ya kitaalamu kwa walezi ili kuboresha huduma za malezi na makuzi ya awali ya watoto, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wataalamu katika sekta hiyo.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Future World Institute, Robert Mkolla, wakati wa mkutano wa wadau wa Umoja wa Vituo vya Kulea Watoto Tanzania (UVIKUWA) uliofanyika Chanika, Dar es Salaam.
Mkutano huo uliandaliwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Kanda ya Saba Chanika, Wilaya ya Ilala, kwa uratibu wa Future World Institute, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa tawi jipya la chuo hicho katika eneo la Chanika kwa Ndevu.
Mkolla amesema mafunzo hayo yanalenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya walezi wenye ujuzi, ambalo limechangiwa na kuongezeka kwa vituo vya kulelea watoto pamoja na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayowafanya wazazi wengi kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji mali.
Amesema programu hiyo inaendana na Sera ya Elimu ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, inayosisitiza umuhimu wa mtoto kupata elimu ya awali kabla ya kuanza darasa la kwanza.

Kwa mujibu wa Mkolla, mafunzo hayo yatawasaidia walezi kupata maarifa kuhusu ukuaji wa mtoto, afya, usalama na mbinu bora za elimu ya awali, jambo litakaloongeza ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya malezi.
Aidha, amesema programu hiyo pia itasaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, hasa wahitimu wa kidato cha nne, kwa kuwapa ujuzi unaoweza kuwawezesha kupata ajira au kujiajiri katika sekta ya malezi ya watoto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVIKUWA, Shabani Kibabi, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuinua viwango vya malezi nchini kwa kuwawezesha walezi kupata taaluma na ujuzi unaohitajika katika kuwahudumia watoto.
Amesema kupitia mkutano huo washiriki pia wamepata elimu kuhusu ujasiriamali na mbinu za kuongeza kipato ili kuboresha uendeshaji wa vituo vyao pamoja na huduma wanazozitoa.
Naye Mwenyekiti wa UVIKUWA Mkoa wa Dar es Salaam, Muhina Mwarabu, amewahimiza walezi na wamiliki wa vituo kutumia fursa hiyo ya mafunzo, akisema ada ya Shilingi 800,000 ni nafuu na itasaidia watu wengi zaidi kupata taaluma ya malezi ya watoto.
Amesema hatua hiyo itachangia kuinua ubora wa huduma za malezi na kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya ukuaji na maendeleo.