
Kikosi cha Simba SC, leo Agosti 5, 2026, kimerejea nchini kikitokea Kigali, Rwanda, kilikoshiriki michuano ya CECAFA Kagame Cup pamoja na maandalizi ya msimu mpya.
Simba ilimaliza safari yake katika michuano hiyo kwenye hatua ya makundi, lakini kocha mkuu Steve Barker amesema ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Barker alisema mashindano hayo yamempa nafasi ya kuwaona karibu wachezaji wote aliokuwa nao kambini na kupata picha ya kikosi chake kuelekea msimu mpya.
Kocha huyo aliongeza kuwa ana imani kubwa na kikosi chake, huku akiwataka mashabiki wa Simba kuendelea kuwa na subira na imani kwamba timu itakuwa na ushindani mkubwa msimu huu.
Wakati huo huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alitamba kuhusu maandalizi ya Simba Day, akiahidi kuwa kutakuwa na mambo makubwa yatakayowafurahisha mashabiki wa klabu hiyo.
Ahmed pia alizungumzia usajili mpya wa kiungo Ibrahim Doumbia, akieleza kuwa mashabiki watajionea ubora wake mara atakapoanza kuitumikia timu uwanjani.