
Savannah James, mke wa nyota wa NBA LeBron James, amesimulia tukio lisilo la kawaida alilokutana nalo katika duka la kifahari la Hermès nchini Italia, baada ya kudai kuwa yeye na rafiki yake walikataliwa kuhudumiwa licha ya kuwa na miadi maalum ya kufanya manunuzi.
Savannah alifichua tukio hilo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Question Everything pamoja na rafiki yake na mshirika wake wa podcast, April McDaniel.
Kwa mujibu wa McDaniel, wawili hao walikuwa kwenye safari ya Ulaya na walikuwa wamepanga mapema kwenda Hermès kwa ajili ya kufanya manunuzi. Hata hivyo, walipofika katika tawi hilo nchini Italia, walidai kuwa mfanyakazi mmoja aliwatendea kwa namna ambayo waliiona kama dharau na hata kujaribu kuwazuia kufanya manunuzi.
Savannah alisisitiza kuwa walikuwa na miadi rasmi, jambo lililomshangaza zaidi kutokana na namna walivyodai kutendewa.

McDaniel, ambaye alisema hakufurahishwa na hali hiyo, alisimama upande wa Savannah na kudai kuwa baadaye mfanyakazi huyo alifukuzwa kazi kutokana na tukio hilo.
Hata hivyo, hali ilibadilika kwa kiasi kikubwa waliporudi dukani. Wawili hao walidai kuwa walipelekwa katika chumba maalum cha faragha na kupewa huduma ya kiwango cha juu, ikiwemo champagne na caviar, huku wakionyeshwa bidhaa mbalimbali za Hermès.
Savannah na McDaniel walieleza kwa utani kuwa baada ya hapo walipewa nafasi ya kuchagua bidhaa nyingi zaidi, huku McDaniel akisema alikuwa tayari kutumia pesa kwa bidhaa mbalimbali.
Tukio la Chanel Nalo Lawaacha Midomo Wazi
Safari yao ya Ulaya haikuishia hapo. Wawili hao pia walidai kukutana na changamoto nyingine katika duka la Chanel nchini Ufaransa.
Safari hii, walidai kuwa mfanyakazi mmoja alimzuia Savannah kugusa begi dogo lililokuwa likionyeshwa dukani, akimwambia mara kadhaa asiliguze.
McDaniel alisema matukio kama hayo hayamfanyi kuacha kununua bidhaa za kifahari, bali humfanya kuchukua hatua kwa kuwasiliana na viongozi wa juu wa maduka husika.
Savannah na McDaniel walieleza matukio hayo huku wakicheka, lakini pia wakisisitiza umuhimu wa wateja kuheshimiwa na kupewa huduma inayolingana na mazingira ya biashara wanayofanya.
Kwa sasa, madai kuhusu mfanyakazi wa Hermès kufukuzwa bado yametolewa na wawili hao, huku taarifa zaidi kutoka kwa Hermès, Chanel au wawakilishi wa Savannah zikisubiriwa.