×

Ushirikiano Imara Unaendesha Mustakabali wa Kilimo Tanzania

Kila tarehe 8 Agosti, Tanzania huadhimisha Nane Nane kwa kutambua mchango wa wakulima katika kulisha taifa, kuimarisha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kilimo ni miongoni mwa sekta muhimu zaidi kwa uchumi wa Tanzania, kikichangia takribani asilimia 26 ya Pato la Taifa (GDP) na kuajiri zaidi ya asilimia 61 ya Watanzania. Sekta hiyo pia hutoa malighafi muhimu kwa viwanda vya chakula na vinywaji, nguo pamoja na bidhaa zinazolenga masoko ya nje.

Hata hivyo, mustakabali wa kilimo hautegemei uzalishaji pekee. Unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wakulima, Serikali, taasisi za utafiti, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo na sekta binafsi ili kuongeza uzalishaji, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya uhakika.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL PLC) inaendelea kushirikiana na wakulima kupitia Mpango wa Smart Agriculture.

Mwaka 2025, TBL ilishirikiana na zaidi ya wakulima wadogo 2,500 kwa kuwapatia ushauri wa kitaalamu, mafunzo ya kiufundi pamoja na programu zinazolenga kuwawezesha kiuchumi.

Ushirikiano huo unalenga kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa mazao na kutumia mbinu endelevu za kilimo, huku ukiimarisha upatikanaji wa malighafi zinazozalishwa nchini.

Dhamira hiyo imeendelea kuimarishwa kupitia Kiwanda cha Kilimanjaro Malting, ambacho kilikamilisha mwaka wake wa kwanza wa uzalishaji mwaka 2025.

 

Kiwanda hicho kinaongeza matumizi ya shayiri inayolimwa nchini na kinatarajiwa kuongeza ununuzi wa shayiri ya ndani pamoja na kupanua fursa za kilimo cha mkataba kwa wakulima wa Tanzania.

Kwa TBL, mafanikio ya wakulima ni sehemu muhimu ya kujenga mnyororo imara wa thamani katika sekta ya kilimo. Wakulima wanapopata maarifa, teknolojia, masoko na fursa za kifedha, wanaweza kuongeza uzalishaji na kujenga biashara za kilimo zenye uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Kwa mantiki hiyo, Nane Nane si wakati wa kutambua tu mafanikio na mchango wa wakulima, bali pia ni fursa ya kutafakari aina ya ushirikiano unaohitajika ili kujenga mustakabali endelevu wa kilimo nchini.

Mustakabali wa kilimo Tanzania unategemea nguvu ya ushirikiano. Kwa kuwaunganisha wakulima, sekta ya viwanda, Serikali, taasisi za utafiti, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo, Tanzania inaweza kuongeza uzalishaji, kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya kilimo na kujenga thamani zaidi katika uchumi wa nchi.

Nane Nane 2026 ni ukumbusho kwamba kilimo ni zaidi ya uzalishaji wa chakula; ni msingi wa uchumi, ajira na fursa za maendeleo. Na msingi huo utaimarika zaidi pale wadau wote watakapofanya kazi pamoja.

Leave a Comment