
Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema timu yake imejiandaa kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, huku akieleza wazi kuwa lengo lao ni kupata ushindi.
Barker ameyasema hayo leo, Agosti 11, 2026, mjini Zanzibar, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Kariakoo Derby hiyo itakayochezwa kesho katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Kocha huyo amesema Simba imefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo na inaingia ikiwa na shauku ya kushinda, huku akisisitiza kuwa klabu hiyo ina malengo makubwa ya kupambania mataji katika msimu huu.
Barker amesema anatambua uzito wa Kariakoo Derby, akieleza kuwa ni mchezo mkubwa unaozikutanisha timu mbili zenye ushindani mkubwa nchini.
Amesema kikosi chake kiko tayari kukabiliana na changamoto ya mchezo huo, huku akiamini maandalizi waliyofanya yatawasaidia kutekeleza mpango wao ndani ya uwanja.
“Tunajua ni mchezo mkubwa na tunaiheshimu Yanga, lakini tumejiandaa kwa ajili ya kupambana na kutafuta ushindi,” amesema Barker.
Kesho, Agosti 12, 2026, kuanzia saa 2:30 usiku, Simba itakuwa na nafasi ya kutafsiri kauli ya kocha wake ndani ya Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mchezo huo wa Ngao ya Jamii utakuwa mtihani mwingine mkubwa kwa Barker mbele ya Yanga, huku lengo aliloliweka wazi likiwa ni kuiongoza Simba kupata ushindi na kuanza msimu kwa mafanikio.
Stori: Kija Z Enock