
Rais wa Marekani Donald Trump amesema alilazimika kubadilisha ndege kwa siri nchini Uturuki mwezi uliopita kufuatia maelekezo kutoka kwa Secret Service, chombo kinacholinda viongozi wakuu wa Marekani.
Tukio hilo lilitokea baada ya Trump kuhudhuria mkutano wa kilele wa NATO mjini Ankara, ambapo alihamishwa kutoka kwenye Air Force One kwenda kwenye ndege ndogo ya kijeshi kupitia gari la kubebea chakula, katika operesheni ya siri iliyolenga kumlinda kutokana na tishio la kuuawa lililoripotiwa kuhusishwa na Iran.
Ikulu ya Marekani haikutoa taarifa kuhusu mabadiliko hayo wakati huo. Siri hiyo ilibainika baada ya The Washington Post kuripoti tukio hilo Jumatatu.
Trump amesema ndege aliyopanda ilikuwa katika hatari zaidi kuliko Air Force One, akieleza kuwa mtu mwenye nia ya kumshambulia angeweza kulenga zaidi ndege ambayo angeamini kuwa ndiyo aliyokuwa akisafiria.

“Nadhani ndege niliyokuwa nimepanda ilikuwa katika hatari zaidi,” Trump aliwaambia waandishi wa habari.
Trump hakusafiri peke yake katika ndege hiyo. Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, baadhi ya wasaidizi wake wa karibu, akiwemo Dan Scavino, Natalie Harp na Walt Nauta, walihamishwa pamoja naye kupitia gari hilo la kubebea chakula.
Hakuna waziri wa Baraza la Mawaziri aliyeripotiwa kuhamishwa pamoja na Trump.
Baada ya tukio hilo kufichuka, mitandao ya kijamii ilijaa picha na vichekesho vikimuonyesha Trump akiwa amejificha kwenye gari la kubebea chakula. Hata hivyo, Trump amesema hakufanya uamuzi huo mwenyewe bali alifuata maelekezo ya Secret Service na jeshi.
Trump pia amesema alifahamu kuwa kulikuwa na tishio, lakini hakutaka kuuliza maelezo mengi, akisema kuwa amekuwa akipokea vitisho vingi.
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu kiwango cha tahadhari za kiusalama zinazochukuliwa kumlinda rais wa Marekani, hasa wakati wa safari za kimataifa.