×

Kikongwe Afa kwa kuliwa na Fisi

Ruvuma: Rest In Peace (R.I.P)! Mahamudu Kilapule (74), mkazi wa Kijiji cha Jiungeni Eneo la Kiweni Mashambani Kata ya Mchesi wilayani Tunduru mkoani hapa, amefariki dunia kwa kushambuliwa kisha kuliwa na mnyama aina ya fisi, akiwa amelala ndani ya nyumba yake.

Akizungumza na gazeti hili, ofisini kwake hivi karibuni, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Revocatus Malimi alisema kuwa, tukio hilo lilijiri Machi 9, mwaka huu, majira ya saa 3:00 usiku kwenye kijiji hicho kilichopo jirani na Mbuga ya Hifadhi ya Wanyama ya Taifa ya Selous.

Kwa mujibu wa Kamanda Malimi, ilidaiwa kwamba, siku hiyo Kilapule, akiwa amelala peke yake kwenye nyumba yake ya nyasi alishambuliwa na fisi huyo aliyesababisha kifo chake.

ACP Malimi ambaye pia ni Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Ruvuma alisema kuwa, majirani walidai kwamba kabla ya kushambuliwa na mnyama huyo, Kilapule alipiga kelele za kuomba msaada ambapo jirani mmoja (hakutaka kutajwa) alikwenda kwenye eneo la tukio kwa lengo la kujua kilichomsibu.

Alisema kuwa, jirani huyo alipofika, alimuona fisi huyo akikimbia kutoka ndani ya nyumba ya Kilapule kuelekea porini na alipoingia ndani ya nyumba hiyo alimkuta Kilapule akiwa amenyofolewa sehemu mbalimbali za mwili na kichwa chake kikiwa kimeliwa na mnyama huyo hivyo kumsababishia umauti.

Kamanda huyo alisema kuwa baada ya kupita muda kidogo, ilidaiwa kwamba fisi huyo alirudi tena kwenye eneo hilo lakini kutokana na wingi wa watu, alikimbilia porini.
Alisema kuwa, hadi sasa polisi wanaendelea kufanya msako mkali wa mnyama huyo kwa kushirikiana na Askari wa Wanyama Pori na wananchi wa vijiji vinavyozunguka kijiji hicho.

Leave a Comment