
Mwanamuziki na mwongozaji maarufu wa vipindi vya televisheni nchini Australia, Johnny Young, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79 baada ya kuugua kwa muda mfupi saratani ya kongosho.
Familia yake imethibitisha kifo hicho leo, Agosti 14, 2026.
Young alijulikana zaidi kama mtayarishaji na mtangazaji wa kipindi maarufu cha televisheni Young Talent Time, kilichoanza mwaka 1971 na kuendelea hadi 1988.

Kipindi hicho kilitoa fursa kwa wasanii wengi chipukizi ambao baadaye walikuja kuwa majina makubwa katika tasnia ya burudani nchini Australia, akiwemo Tina Arena na Dannii Minogue.
Mbali na kazi za televisheni, Young alikuwa mwanamuziki, mtunzi wa nyimbo na mtayarishaji wa muziki. Alihusika katika kutengeneza nyimbo maarufu kama “The Real Thing” na “Smiley”, huku mchango wake katika muziki na televisheni ukimfanya kuwa mmoja wa watu muhimu katika historia ya burudani ya Australia.

Mchango wake katika tasnia ya muziki ulitambuliwa mwaka 2010 alipoingizwa katika ARIA Hall of Fame.
Baada ya taarifa za kifo chake, viongozi na wasanii mbalimbali nchini Australia wametoa salamu za pole na kumkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika kukuza vipaji vya vijana.
Stori na Ashura Karimu | GPL